Wednesday, September 3, 2014

Zanzibar kufaidika na ubunifu mpya wa Zantel

Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Kampuni ya simu za mkononi ya Zantel kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) imezindua huduma mpya ya kununua umeme wa TUKUZA kupitia EzyPesa.

“Tunafuraha kubwa leo kuzindua huduma hii kwa wateja wa ZECO na Zantel kwa ujumla… hakika itawapa thamani ya pesa zao, urahisi wa kununua  umeme pamoja na faraja ya huduma bora kwa wateja,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Zantel, Bw. Pratap Ghose wakati wa uzinduzi huo hivi karibuni mjini Unguja.

Alisema uzinduzi huo utawawezezesha Wazanzibari kufurahia ununuzi wa umeme kwa njia iliyo bora na yenye wepesi zaidi ambapo wateja wa ZECO wataweza kununua umeme wakati wowote na pahala popote.

Aidha wateja wa Zantel wataweza pia kununua na kupata huduma nyengine mbali ya umeme kwa kupitia EzyPesa.

“Huduma hii itapatikana kwa wateja wa Zantel waliojiunga na EzyPesa ambao usajili wake unapatikana kwa urahisi kabisa kupitia wakala wa EzyPesa,” alisema.

Alieleza kuwa sera ya utoaji wa huduma zilizo bora kumfikia mwananchi pahala popote alipo na kwa wakati wowote ndiyo iliyozalisha wazo la kushirikiana katika kusambaza huduma ya TUKUZA kwa kutumia mtandao wa Zantel ndani ya mfumo wa EzyPesa.

Bw. Ghose alisema kuwa huduma ya EzyPesa inakwenda sambamba na matarajio na uwekezaji wa kampuni ya Zantel wenye lengo la kuifanya kampuni kuwa ya kwanza kwenye utoaji wa huduma hiyo kwa Zanzibar.

Alisema ni jukumu la Zantel na ZECO kama kampuni za Zanzibar,  kuwahakikishia Wazanzibari sio tu huduma nzuri lakini huduma zinazoweza kuwapa fursa mbali mbali za kijamii na kiuchumi.

Alisisitiza kuwa mteja aliye na Zantel, sasa anaweza kupata  huduma zote  za malipo ikiwa ni pamoja na taratibu zote za  Kodi , Ushuru, Leseni za Biashara, Mifuko ya Jamii, Huduma za Kibenki zimeunganishwa  Kupitia Huduma ya EzyPesa.

Pia Kupitia Huduma ya EzyPesa, mashirika binafsi na kampuni za umma zinaweza kulipa ankara  mbalimbali na mishahara ya wafanyakazi  kwa uhakika na usalama.

Akizungumza na waandishi mara baada ya kufanya uzinduzi wa kihistoria wa huduma mpya ya kununua umeme wa TUKUZA kupitia EzyPesa Waziri wa Ardhi, Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar alisema huduma hii imekuja wakati mwafaka ambapo kulikuwa na shida ya upatikanaji wa huduma ya kununua umeme wa TUKUZA kupitia mawakala.
“Alisema kwa sasa tatizo la kupangafoleni kwa mawakala wa umeme litakwisha kwa kupitia huduma hii mpya ya kununua kupitia simu ya mkononi kupitia mtandao wa Zantel”.

Alisema kupitia makubaliano haya mwananchi watanufaika kwa huduma hii kwani ni rahisi kutumia na hivyo itapelekea kuona thamani ya pesa zao.

Zaidi amewataka wananchi kuondoa wasiwasi juu ya bei za umeme kwmba gharama za kununua umeme zitabaki kuwa zilezile kwani makubaliano ni ya zantel na zeco hivyo wananchi hawataathirika kwa kuhofia gharama kupanda.

Alisisitiza kwamba wananchi wanatakiwa kununua umeme kulingana na matumizi kwani kunawengine wanamatumizi makubwa kuliko kiwango wanacho nunua hivyo wanaweza hisi wameibiwa au kunagharama za ziada wakati wa kununua umeme kwa hii huduma mpya.

“Gharama za umeme zipo vilevile zaidi wananchi wanatakiwa kununua kulingana na matumizi” alisema

Kwa upande wake meneja wa ZECO Bw. Hassan Ally Mbarouk alisema awali wananchi walitakiwa kufika kwenye vituo za umeme na pia vilikuwa kwa muda  maalum sasa kupitia huduma hii wananchi wataokoa muda wao kwa kununua umeme kupitia EzyPesa.

Pia Bw. Hassan alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kujiunga na huduma ya EzyPesa ili kupata fursa za kununua umeme kupitia simu zao wakati wowote.

Uzinduzi huo wa kihistoria ulifanywa na Waziri wa Ardhi, Makaazi Maji na Nishati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Ramadhan Abdalla Shaaban.


Mwisho.

No comments: