Wednesday, September 10, 2014

TNBC yazipa changamoto halmashauri mkoani kuibua fursa za kibiashara

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Bw. Raymond Mbilinyi akisisitiza jambo wakati wa Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni.Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulijadili  namna ya kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji katika halmashauri za mkoa huo, kujenga ushirikiano wa pande mbili kati ya sekta ya umma na binafsi. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu na (katikati) ni Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo mkoani humo( TCCIA), Bw.Yohana Nchimbi, mkutano huo.
Baadhi ya wajumbe wa baraza la biashara la mkoa wa Ruvuma wakifuatilia kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zinatolewa Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni.Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulijadili  namna ya kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji katika halmashauri za mkoa huo, kujenga ushirikiano wa pande mbili kati ya sekta ya umma na binafsi
Na Mwandishi Wetu, Songea

Halmashauri  mkoani Ruvuma zimepewa changamoto kujitathimini kutokana na kuibua fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo katika maeneo husika na kuzitangaza iliziweze kuwavutia wawekezaji zaidi.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ,Bw. Raymond Mbilinyi alitoa wito huo kwa wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni mjini hapa kuwa wakati umefika kwa halmashauri kuweza kuyaainisha maeneo yote muhimu yenye fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji.

“Mkutano huu na wadau wote wa baraza ambao unawajumuisha wajumbe kutoka halmashauri zote za mkoa huu ni vyema mnapo rudi kwenye maeneo yenu ya kazi mkafanya mnyakato wa kuainisha fursa zote,” alisisitiza Bw. Mbilinyi.

Alisema baraza linaamini endapo halmashauri zitaibua fursa za biashara mapato ya serikali yataongezeka pia ajira kwa vijana zitaimarika hivyo kipato kwa watanzania kitakua pia.

aliwambia waandishi wa habari mkoani humo muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa kiako cha baraza la biashara la mkoa wa ruvuma kuwa  vivutio vingi katika sekta za utalii, kilimo na madini, vinaweza kuubadilisha taswira ya mkoa wa huo kwa kipindi kifupi.

“Huu mkoa unakila sababu za kujivunia katika uzalishaji wa mazao ya  chakula na biashara kwani una ardhi ya kutosha yenye rutuba na mvua ya kutosha pia,” alisema na kusisitiza kuwa hivyo vyote vitumike kubadilisha maisha ya watu na kukuza kipato.

Alisema mbali na Kilimo, Mkoa wa Ruvuma una  madini ya Uranium,  makaa ya Mawe na maeneo mazuri ya kuvutia utalii wa ndani na nje ya nchi.

 “ Mkoa huu ni tajiri sana, kila kitu kipo jambo kubwa ni kwa watendaji wa  halmashauri kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuvutia zaidi  uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kubadilisha maisha ya watu,” alisema

Alisema kuwepo kwa baraza la mkoa ambalo linajuisha wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi  litakuwa chachu kubwa ya kuongeza kasi ya kimaendeleo katika wilaya zote mkoani hapa.

“Kikao hiki kitakuwa ni mwongozo tosha katika kuwekana sawa , tumejadili mambo mengi ya msingi na pia naamini kuwa baada ya muda mfupi kutakuwa na  matokeo mazuri,”alisisitiza.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi, alisema wilaya yake inategemea sana uvuvi ili kuingiza kipato katika halmashauri hiyo na kusema kuwa lengo lao kwa sasa ni kuwawezesha vijana kwa kuwapatia zana za kisasa za kuvulia samaki.

“Vijana wetu wamekuwa wakitumia uvuvi wa kienyeji sana lakini kwa sasa tumeagiza boti za kisasa ili waweze kuvua kisasa zaidi,” alisema

Ameongeza kuwa walikuwa wanatumia mitumbwi jambo ambalo lilikuwa linahatarisha maisha yao, kutokana na kutokuwa na uimara na viwango vya kutosha wawapo ziwani.

“ Kwa kweli tumefanikiwa katika hili vijana pamoja na akina mama waliokuwa wanasumbuka watakuwa salama na kipato kitaongezeka katika kaya,” alisema Kahindi

Nae mwenyekiti wa chama cha wenye viwanda biashara na kilimo ( TCCIA) wilaya ya Tunduru Mohamed Kiondo alisema Baraza hilo limewapa mwanko katika kuhimiza suala la kilimo katika wilaya zao, kwani ndio kitu pekee kitakachomkombo mwananchi wa Ruvuma.

“Mkoawetu uantegemea kilimo, tuna tumbaku, korosho pamoja na zao la mahindi haya ni mazao makuu na yanaingiza pesa nyingi, baraza hili I fursa pekee ya kujitangaza,” alisema Kiondo.

Aliongeza kuwa yanayojadiliwa katika vikao vya mabaraza ya mikoa pamoja na wilaya yanatakiwa kufanyiwa tathimini ya hali ya juu ili kuleta matokeo chanja katika kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Mwisho


No comments: