Friday, September 12, 2014

Matumizi sahihi ya raslimali muhimu kuleta mabadiliko chanya--Kikwete

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Rais Jakaya Kikwete amesema jana kuwa Tanzania inatakiwa kuchukua hatua za makusudi katika matumizi ya raslimali zake na kuratibu kwa makini shughuli za wadau mbalimbali ili kufikia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayotakiwa.
Alikuwa akifungua mkutano wa Tatu wa Kitaifa wa Taasisi ya utafiti ya maswala ya Jamii na Uchumi (ESRF) jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo uliangazia fursa za ukuaji na mabadiliko ya kiuchumi kwa maendeleo ya watu Tanzania.

Rais Kikwete alisema mada ya mkutano huo iliendana na mahitaji na hali ya sera zinazoongoza nchi kwasasa akisema kuwa Dira ya Maendeleo ya 2025 inalenga kuibadili nchi kutoka uchumi mdogo hadi kufikia uchumi wa kati wenye maisha bora zaidi, amani, utengamano, umoja na utawala bora miongoni mwa mambo mengine.

“Mkutano huu utasaidia kutathmini kama tuko katika njia sahihi katika kufikia lengo hilo,” alisema.

Rais alisema mabadiliko hayo yatajionyesha kwa kupungua kwa utegemezi wa sekta ya kilimo na kuongezeka kwa uzalishaji na sekta ya huduma kadiri muda unavyokwenda.

“Uchumi utakuwa haraka kama uzalishaji na sekta ya huduma ambavyo kwa kiwango kikubwa vinategemea maarifa na teknolojia vitakuwa kwa haraka kuliko kilimo,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa mipango iliyopo ni kuwa sekta ya viwanda inategemewa kukua kutoka asilimia 24.4 hadi asilimia 30.7 mwaka 2025 wakati ile ya huduma inatarajiwa kuongezeka kido hadi asilimia 48.6 toka kiwango chake cha asilimia 47.8 mwaka 2010.

Rais alifafanua kuwa mpango wa pili wa miaka mitano ya maendeleo ((2016/17-2020/21) utalenga kuimarisha uchumi wa viwanda.

“Msisitizo utakuwa kwenye viwanda vya gesi asilia, kilimo na teknolojia,” alisema.

Alitaja baadhi ya maendeleo yaliyofikiwa na serikali kama kuongezeka kwa kiwango cha maisha kutoka miaka 51 mwaka 2002 hadi miaka 61 mwaka 2012 na kupungua kwa vifo vya watoto kutoka vifo 91.6 hadi 51 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya ESRF, Bw. Philemon Luhanjo alisema taasisi hiyo imefanya kazi kubwa ya kujenga uwezo wa utafiti na uchambuzi wa sera mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.

“Changamoto kubwa tuliyonayo si tu ya maendeleo bali ya mabadiliko…lazima tuhakikishe kuwa kukua kwa nchi yetu kunaendana na ustawi wa watu,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dr. Hoseana Lunogelo alisema kuwa ni muhimu sana kwa Tanzania kuendeleza watu wake ili kupambana na changamoto za maendeleo zilizopo.

“Kwa kuwekeza katika maendeleo ya watu, serikali itawawezesha wananchi wake kuendesha maisha yao na kuwa na faida kwa jamii,” alisema.
Mkutano huo ulihudhuriwa wa wadau mbalimbali wakiwemo wasomi, sekta binafsi, ya umma na wadau wa maendeleo.

Mwisho


No comments: