Muanzilishi wa kampuni ya Original Water, mzalishaji wa maji
ya Eden Mineral Water, Prof. Hulda Swai akionyesha chupa ya maji hayo alipokuwa
akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam. Maji hayo yanatengenezwa na madini muhimu
yanayopatikana katika chumvi toka milima ya Himalaya. Kushoto ni Mkurugenzi wa
kampuni hiyo, Bi. Asenath Mpatwa.
Na Mwandish Wetu, Dar es Salaam
Watanzania wametakiwa kuhakikisha kuwa wanakunywa maji
safi, salama na yenye madini yanayotakiwa ili kulinda afya zao.
Ushauri huo umetolewa na Mwanasayansi anayejulikana
kimataifa, Prof. Hulda Swai alipokuwa akiongea na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam.
Profesa huyo Mtanzania anayefanya kazi katika Chuo
Kikuu cha Pretoria nchini Afrika ya Kusini amesema maji yanayofaa kwa matumizi
ya binadamu ni yale yenye viwango vinavyotakiwa vya madini.
“Maji si maji tu...maji ni yale yenye madini
yanayotakiwa na mwili,” alisema.
Akifafanua zaidi alieleza kuwa yeye kama mwanasayansi
amegundua kuwa maji mengi yanayotumika ni maji “mfu” ambayo hayana madini
yoyote na kuwa hiyo inasababishwa na mchakato wa kuchuja maji hayo.
Alisema kutokana na uchafuzi wa mazingira uchujwaji wa
maji unaofanyika huondoa madini mabaya na yale mazuri na hivyo kufanya maji
hayo kutokuwa na faida iliyokusudiwa mwilini.
Ni kutokana na hilo, Prof. Swai
anasema amekuja na teknolojia mpya itakayosaidia kuchuja maji na kuongezea
madini yanayotokana na chimvi kutoka milima ya Himalaya ambayo ina aina ya
madini asilimia 84 kama inavyotakiwa na mwili wa binadamu.
Amesema maji hayo yanayojulikana
kama Eden Mineral water yana kiwango sawa maji yaliyotumiwa na mababu na hivyo
kuwa na uwezo wa kusaidia mwili kuwa na uwezo wa kupambana na magonjwa na
kusafishwa mwili.
“Babu zetu walikunywa maji yenye
viwango vizuri sana vya madini na ndio maana hawakupata sana magonjwa kama
sasa,” alisema.
Alisema wanatumia teknolojia mpya
kabisa kuchuja maji hayo kabla ya kuweka kitaalamu madini yanayotokana na
chumvi hiyo ambayo bado haijaharibiwa na uchafuzi wa mazingira.
“Tunatumia teknolojia mpya kabisa
ya nano filters 0.1nm...hapa hakuna chembechembe zozote zinazoweza kupenya
isipokuwa maji,” alisema Prof. Swai ambaye ni muanzilishi wa kampuni ya
Original Water inayotengeneza maji hayo.
Akitaja baadhi ya faida za maji hayo, Prof.
Swai alisema maji yanasaidia mwili kufyonza viinilishe kutoka katika chakula
tunachokula na kuvisafirisha sehemu mbalimbali za mwili na kuweka kiwango cha
alkali mwilini kinachotakiwa.
Alisema pia kutokana na madini
yanayopatikana katika chumvi hiyo, maji hayo yana sifa zinazosaidia seli za
mwili kuwasiliana kama inavyotakiwa.
“Maji haya pia yanasaidia kupunguza uzito
wa mwili, usagaji mzuri wa chakula na kuhifadhi nguvu ya mwili inayotakiwa,”
alisema.
Mkurugenzi wa kampuni ya Original Water inayotengeneza
maji hayo ya Eden Mineral water, Bi. Asenath Mpatwa alisema maji hayo yamepata
muitikio mzuri tangu yaanze kuuzwa na kuwa watu wameanza kufahamu faida zake.
Aliipongeza serikali kwa kuwa na sera inayoruhusu watu
binafs kutengeneza maji.
Alisema kampuni yao imesajiliwa na maji hayo yamekaguliwa
na kupata idhini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA).
“Sekta ya maji ni moja ya sekta muhimu...maisha ya
binadamu yanategemea maji na maji ya kunywa ni muhimu zaidi katika kuendeleza
uhai,” alisema Bi. Mpatwa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment