Friday, August 29, 2014

Urasimu utoaji vibali vya ujenzi kikwazo kwa maendeleo -TPSF

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye akizungumza wakati wa warsha ya kujadili ripoti ya mshauri mwelekezi kuhusu uboreshaji utoaji wa vibali vya ujenzi hapa nchini jana jijini Dar es Salaam.  Warsha hiyo inayomalizika leo imetayarishwa na TPSF.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) akisisitiza jambo kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Bw. Kagyabukama Kiliba wakati wa warsha ya kujadili ripoti ya mshauri mwelekezi kuhusu uboreshaji utoaji wa vibali vya ujenzi hapa nchini jana jijini Dar es Salaam.  Warsha hiyo inayomalizika leo imetayarishwa na TPSF.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) imesema Tanzania haiwezi kuendelea kukwamishwa na urasimu wa utoaji wa vibali vya ujenzi ambavyo vinarudisha nyuma juhudi za kujenga mazingira bora ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye amesema hivyo jana wakati wa warsha ya kujadili ripoti ya mshauri mwelekezi kuhusu uboreshaji utoaji wa vibali vya ujenzi hapa nchini.

“Suala la utoaji vibali vya ujenzi limekumbwa na changamoto ya urasimu ambao unachelewesha kupata vibali vya ujenzi na kusababisha hasara kwa sekta binafsi na kwa taifa,”alisema jana jijini Dar es Salaam.

Alisema ili nchi iweze kuondokana na changamoto hiyo inahitaji kuboresha mazingira ya usimamizi wa ardhi pamoja na utoaji wa vibali vya ujenzi.

Kwa sasa juhudi kubwa zinafanyika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje lakini wanapokuwa tayari kujenga wanachukua miaka mingi kupata kibali cha ujenzi.

Alisema ucheleweshaji huo pia unasababisha kupoteza ajira, na fursa ya kutumia majengo yaliyokusudiwa kujegwa kama njia ya kuleta maendeleo.

Akitoa mfano alisema nchi jirani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepiga hatua kubwa katika utoaji vibali hivyo kwa njia ya mtandao.

“Ni lazima tubadilike, wawekezaji tunaovutia ni hao hao,” alisema.

Alisema mpango elekezi wa kuboresha mazingira ya biashara unaosimiwa na Ofisi ya waziri Mkuu uliainisha upatakanaji wa vibali vya ujenzi kama eneo linalohitaji kuboreshwa na kuundiwa kikosi kazi cha serikali ambacho kilishirikisha sekta binafsi.

Kwa kutambua hilo sekta binafsi iliamua kuunda kikosi kazi chake ambacho kilikuwa kinafuatilia utekelezaji wa maboresho yaliyoainishwa kwenye mpango huo na kilifanya tafiti ya changamoto ya upatakanaji wa vibali hivyo.

“Kikosi kazi hiki kimekuja na ripoti ambayo tunaijadili hapa na tutatoa mapendekezo ya jisni ya kuzipunguza changamoto za ucheleweshaji utoaji vibali,”alisema.

Mkutano huo unamalizika leo.  

Alisema mapendekezo hayo baada ya kutolewa yatapelekwa serikali ili waweze kuyafanyia kazi na kuiondosha changamoto hiyo na changamto zingine ambazo nchi haifanyi vizuri kulingana na ripoti ya dunia inayotolewa kila mwaka.

Awali, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, Bw. Kagyabukama Kiliba alisema hatua ya sekta binafsi kuandaa ripoti na kuijadili ni hatua ya msingi katika kujenga ushirikiano na serikali katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za kuboresha uwekezaji.

“Nawahakikishia sisi kama serikali tutayachukua mapendekezo yenu na kwenda kuyafanyia kazi kwa nia ya kuzidi kujenga mazingiara bora ya utoaji vibali vya ujenzi,”alisema.

Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ndiyo inayohusika na utekelezaji wa mpango elekezi wa kuboresha mazingira ya biashara katika kiashiria cha vibali vya ujenzi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Civil Engineering Contractors Association (TACECA), Bw. Clement Mworia alisema utoji wa vibali umekuwa ni tatizo kubwa katika sekta ndogo ya ujenzi na hiyo inarudisha nyuma maendeleo yake.

“Kumekuwepo na hali ya kuporomoka kwa majengo hapa nchini hasa Dar es Salaam, hii inasabishwa na urasimu wa utoaji vibali ambapo watu wanajenga bila ya halmashauri kukagua msingi wa ujenzi,”alisema.
Warsha hiyo inashirikisha wajumbe toka sekta binafsi na umma.

Mwisho. 


No comments: