Meneja wa benki ya Afrika
Tanzania, tawi la Mtwara, Bw. Godfrey Chilewa (kushoto) akikabidhi vitabu kwa
mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya Bandari, Mtwara, mwishoni mwa wiki, Bi.
Somoe Ismail. Benki hiyo ilitoa msaada wa vitabu 118. Chombo hicho
cha fedha kiko katika kampeni ya kusaidia sekta ya elimu nchini.
Na Mwandishi wetu, Mtwara
Benki ya Afrika Tanzania imeendelea na juhudi zake za kusaidia
sekta ya elimu hapa nchini.
Katika tukio la hivi karibuni, benki hiyo tawi
la Mtwara imetoa msaada wa vitabu 118 kwa shule ya sekondari ya
Bandari mkoani humo lengo likiwa kusaidia juhudi za serikali katika kuboresha
shule za umma.
Meneja wa benki hiyo, Bw. Godfrey Chilewa amesema mwishoni mwa
wiki mkoani humo kuwa kwa mwaka huu wamelenga kusaidia vitabu vyenye thamani ya
Tshs milioni 15 katika shule mbalimbali nchini na kwa miaka ijayo wataangalia
miundombinu mingine.
Shule ya sekondari ya Bandari ni mpya na inakabiliwa na changamoto
nyingi vikiwemo vifaa vya kufundishia pamoja na miundombinu.
“Shule nyingi za umma zina changamoto nyingi ambazo zinatokana na
uwezo wa serikali wa nchi zinazoendelea kushindwa kumudu kwa asilimia
100 gharama zote za maendeleo ikiwemo elimu,” alisema.
kwa upande wake, mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Somoe
Ismail aliishukuru benki hiyo kwa msaada huo na kuomba wafadhili wengine
kujitokeza kuisaidia shule hiyo ambayo ni mpya na ina kidato cha kwanza
pekee huku ikiwa inakabiliwa na changamoto nyingi.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na uchache wa madarasa
ambapo shule hiyo kwa sasa ina madarasa manne na wastani inatakiwa kuwa na
madarasa kumi na sita, ukosefu wa maabara na vifaa vyake na madawati.
Naye, afisa elimu taaluma sekondari manispaa ya Mtwara,
Bw. Juma Chikonjo alisema sehemu kubwa ya shule sekondari katika manispaa hiyo
zinakabiliwa na changamoto nyingi.
Hivyo ametoa wito kwa taasisi zingine kusaidia changamoto hizo
ikiwemo ujenzi wa maabara ambapo amesema kati ya shule 13 za serikali
zilizopo katika manispaa hiyo ni shule sita tu ndiyo maabara zake zimekamilika.
Hata hivyo ametaka wanafunzi wa shule hiyo kuvitumia vitabu hivyo
kwa manufaa yao ya baadae.
Vitabu vilivyotolewa ni vya masomo yote yakiwemo masomo ya
sayansi.
kwa upande wa wanafunzi wa shule hiyo ambao wapo 70
wamefurahia msaada huo na kusema kuwa vitawasaidia na kuahidi kusoma kwa bidii.
Mwisho
No comments:
Post a Comment