Monday, August 25, 2014

UWADAR, DARCOBOA wafikia makubaliano na Simon Group

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Umoja wa wasafirishaji Dar es Salaam (UWADA) na Umoja wa Wamiliki wa Mabasi ya Abiria Dare s Salaam (DARCOBOA) wametiliana saini ya makubaliano na viongozi wa kampuni ya Simon Group kunganisha nguvu ili kuwa na nguvu ya kushiriki katika mchakato wa kuomba zabuni ya watoa huduma katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).

Makubaliano hayo yalifanyika mwishoni wa juma jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI,Bi. Hawa Ghasia, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Meck Sadick na Mtendaji Mkuu wa mamlaka ya DART, Bi. Asteria Mlambo.

Wakati UWADAR iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Bw. William Masanja; huku DARCOBOA ikiwakilishwa na Mwenyekiti wake pia, Bw. Sabri Mabruk.

Simon Group iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Bw. Robert Kisena. 
Simon Group ndiyo inayoendesha Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Katika halfa hiyo, Waziri Ghasia alisema makubaliano hayo ni hatua muhimu kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri jijini kuwa na nguvu ya pamoja na kujenga uwezo wa kuingia katika mfumo wa wa DART ambao unahitaji ufanisi mkubwa katika utoaji huduma.

“Uamuzi wenu ni mzuri...nawapongeza,” alisema.

Alifafanua kuwa serikali kupitia DART kwa sasa ipo katika hatua ya kutafuta watoa huduma katika mfumo huo na inatarajia kutangaza zabuni ambazo kampuni mbalimbali za ndani na nje zitatakiwa kuomba.
Alisema mfumo huo hauruhusu mmiliki mmoja mmoja bali kwa kupitia kampuni yenye sifa.

Alifafanua kuwa kipaumbele cha serikali ni kuona watanzania wanashiriki katika uwekezaji ili kuzidi kujenga uchumi na kuleta maendeleo. 

Naye Bw. Mabruk alisema serikali iliwashirikisha kikamirifu katika mchakato mzima tangu mradi ulipoanza hadi sasa unapoelekea kukamilika kwa awamu ya kwanza.

“Turishirikishwa tangu mwanzo na tulipelekwa hadi nje ya nchi katika mji wa  Bogota kujifunza jinsi wenzetu wanavyoendesha,”alisema.

Alisema jambo hilo haliepukiki kwa sababu ndiyo maendeleona kuwa wamiliki wa daladala wako tayari kushirikiana na kampuni hiyo ya UDA ili kujenga nguvu zaidi.

Alisema wamefanya maamuzi hayo kwa hiari na kila mmiliki atakayependa kuingia kushirikiana na kampuni hiyo atafanya kwa hiari kulingana na makubaliano yaliyofikiwa.

Naye, Bw. Kisena alisema shirika lake linapongeza hatua hiyo ambayo itawafanya kuwa na nguvu moja na kuwa washindani.

“Hatua hii itatuwezesha kuwa na nguvu ya kuwa washindani,” alisema.
Alisema kampuni yake inatoa fursa kwa wamiliki wa daladala kununua hisa za kampuni yao ili waweze kuwa ni sehemu ya ya kampuni hiyo.

Alisema pia shirika hilo litatoa fursa ya kwa watanzania wa kawaida wanaotaka kuwa sehemu ya kampuni yao kununua hisa ili waweze kuwa ni sehemu ya kampuni kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Sadick alisema jambo hilo ni jema na linalenga wazawa kuwa na mwelekeo wa pamoja ili kuwekeza kwa kushirikiana na wataalamu wa kigeni.

Mwisho


No comments: