Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Bw. Raymond Mbilinyi (kulia) akizungumza na wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Iringa kwenye mkutano wa siku moja uliowakutanisha wajumbe wa sekta ya umma na binafsi na kuzungumzia namna ya kuimarisha mazingira bora ya biashara na uwekezaji mkoani humo hivi karibuni. Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Ramadhani Mungi (kushoto).
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr.
Christine Ishengoma akizungumza jambo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la
Biashara (TNBC) Bw. Raymond Mbilinyi baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku
moja wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Iringa hivi karibuni. Mkutano huo
uliwakutanisha wajumbe kutoka sekta ya umma na binafsi na kuzungumzia namna ya
kuimarisha mazingira bora ya biashara na uwekezaji mkoani humo.
Na Mwandishi
Wetu, Iringa
Baraza la Taifa
la Biashara (TNBC) limewataka watendaji wa halmashauri zilizopo katika mkoa wa
Iringa kuimarisha mazingira ya uwekezaji ili kuweza kuwavutia wawekezaji wengi
wa ndani na nje ya nchi.
Katibu Mtendaji
wa Baraza hilo, Bw. Raymond Mbilinyi amesema mkoani humo wakati akizungumza na
wajumbe wa baraza la biashara la mkoa wa Iringa juu ya mikakati mbalimbali ya
kuimarisha uchumi na kujenga mazingira bora ya biashara katika mkoa huo.
“Watendaji siku
zote ndio wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kusaidia serikali katika suala la
uwekezaji katika halmashauri zao,” alisema Mbilinyi.
Alisema kazi
kubwa ya baraza ni kuunganisha sekta binafsi na ile ya umma kuhakikisha
wanafanya kazi pamoja hivyo ni jukumu la watendaji wa ngazi za juu katika
halmashauri hizo kujenga mazingira bora ya biashara ili kuvutia wawekezaji
wengi.
“Bila kuboresha
mazingira, hamna biashara wala uwekezaji,” alisema.
Alisisitiza
kuwa Baraza litaendelea kukutana na wajumbe wa upande wa sekta ya umma na
binafsi ili kujadiliana kama kuna vikwazo vyovyote katika ufanyaji biashara ili
kuweza kuvitatua kama si kuviondoa kabisa.
“kumekuwa na
vikwazo katika ufanyaji biashara hivyo mikutano kama hii ni muhimu sana katika
kutatua kero mbalimbali,” alisisitiza Bw. Mbilinyi.
Akielezea
umuhimu wa mabaraza hayo, alisema ni mkubwa kwa kuwa wajumbe wa pande zote
mbili hukutana na kutoka na kauli moja ya kutatua kero ambazo zipo katika
biashara na kuzifanyia kazi kwa kina ili kuondoa migogoro katika sekta hiyo.
“Kukiwa na
migongano kwa pande hizi mbili hatuwezi kwenda na ndio maana tunakaa pamoja ili
kujua kuna kero gani katika sekta zetu za kukuza uchumi kwenye mkoa,” alisema.
Kwa upande
wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa DKT. Christine Ishengoma aliishukuru TNBC kwa
jitihada zake za kuunganisha sekta hizo mbili ili kuweza kufanya kazi pamoja
lengo likiwa ni kuendeleza mkoa wake.
“Mimi niseme
kwamba TNBC wanajitahidi sana katika kutuunganisha, naomba waendelee na kazi
hiyo ya kujenga nchi,” alisema Dk. Ishengoma.
Alisema mkoa
wake una vivutio vingi vya uwekezaji na kuwa kinachotakiwa ni kuwekewa
mazingira bora ya kufanya biashara ili wawekezaji wengi wawekeze Iringa kwani
kwa kufanya hivyo mkoa utaweza kukua kiuchumi.
“Tuna utalii,
kilimo pamoja na ufugaji hivi vyote ni vivutio vikubwa sana vya uwekezaji,”
aliongeza.
Aidha aliwataka
watendaji kuacha urasimu usiokuwa wa lazima kwani unakwamisha juhudi za
serikali za kuondoa umasikini kupitia uwekezaji hasa pale mwekezaji anapohitaji
ardhi kwa ajili ya uwekezaji.
“Mimi nashanga
sana mwekezaji anaweza kuzungushwa karibu mwaka mzima kwa kitu cha siku nne
mpaka tano naomba tubadilike,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment