Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji,
Dkt. Mary Nagu (katikati) akiingia katika kongamano la majadiliano kuhusu
changamoto za kufikika kwa huduma za fedha kwa wajasiriamali wadogo na wa kati
Tanzania jijini Dar es Salaam Jumanne wiki hii.
Wengine ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Bw.
Raymond Mbilinyi (kushoto) na Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye
(Kulia). Kongamano hilo lilitayarishwa
na TPSF pamoja na Mfuko
wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi za fedha nchini zimeshauriwa kulegeza masharti ya utoaji mikopo
ili wajasiriamali nchini waweze kupata fursa zaidi ya kupata mitaji kuendeleza
biashara zao na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa nchi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary
Nagu alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kufungua Kongamano la majadiliano kuhusu changamoto za kufikika kwa huduma za
fedha kwa wajasiriamali wadogo na wa kati Tanzania jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo alisema Jumanne wiki hii kuwa taasisi za fedha nchini
zilegeze masharti ili wajasiliamali waweze kupata mitaji ya biashara zao.
Kongamano hilo lilitayarishwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania
(TPSF) kwa kushirikiana na Financial Sector Deepening Trust (FSDT).
“Ninayo furaha kubwa kuona TPSF na wadau wengine wameandaa kongamano
hili ambalo linalenga kutafuta suluhisho la wajasiliamali kupata mitaji kutoka
taasisi za fedha,”alisema.
Alisema moja ya changamoto ambazo wajasiriamali wanakumbana nazo ni
namna ya kupata mitaji kutoka katika taasisi hizo, jambo ambalo linarudisha
nyuma maendeleo ya biashara.
Alisema mikopo kutoka benki inatolekewa kwa masharti makubwa na riba
kubwa jambo ambalo ni kikwzo kwao na taifa pia.
“Sera ya nchi inaruhusu sekta binafsi kuendesha uchumi kupitia kampuni
ndogo, za kati, na wajasilimali, sasa mitaji kwa wajasiriamali ni jambo ambalo
haliepukiki,”alisema.
Alisema serikali inashirikiana na TPSF kuhakikisha mazingira ya biashara
yanaimarika na kongamano hilo ni moja ya hatua muhimu katika kuondoa vikwazo
hivi.
Aidha alisema wakati nchi inasubiri kuingia katika uchumi mkubwa
kutokana na gesi na mafuta ni lazima wajasiriamali wadogo wawezeshwe ili pia
wawe na uwezo wa kutoa huduma kwa kampuni kubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji TPSF, Bw. Godfrey Simbeye alisema
kongamano hilo ni la muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa mitaji kwa
wajasiliamali ambao ni tegemeo kubwa katika kuendeleza nchi.
“Nchi zilizofanikiwa zimewekeza katika maendeleo ya wajasiriamali wao,
hatuna budi kufanya hivyo,” alisema.
Alifafanua kuwa wajasiriamali wakipatiwa huduma za fedha na kukuza
mitaji yao, wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo..
“Tumeshuhudia ukuaji wa mitaji na uchumi wetu unakwamishwa na mambo
mengi mojawapo ni namna ya kupata mitaji,”alisema.
Alisema mitaji mingi inatoka benki lakini kwa mazingira
yaliyopo ni vigumu kwa biashara inayoanza kupata mitaji kutokana na masharti
ambayo siyo rafiki.
Alisema sekta hiyo lazima iwezeshwe sababu ndiyo yenye uwezo wa kutoa
jira kubwa na kuleta mapinduzi ya uchumi.
Naye Mtaalamu wa Maswala ya Wajasilimali, kutoka FSDT, Bw. Peter Kingu
alisema kuna kila sababu taasisi za fedha kupanua wigo kwa wajasilimali kupata
mitaji bila ya kuweka masharti magumu.
“Taasisi yetu inafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo
TPSF katika kuhakikisha wajasiriamali wanaimarika kibiashara,” alisema.
Kongamano hilo lilishirikisha wadau mbalimbali toka sekta binafsi, sekta
ya umma, taasisi za utafiti, kampuni mbalimbali pamoja na benki miongoni mwa
wadau wengine.
Kampuni ya simu za mkononi ndiyo iliyodhamini kongamano hilo.
Inatarajiwa kuwa maazimio ya kongamano hilo yatasaidia katika juhudi za
kurahisisha upatikanaji wa huduma za fedha miongoni mwa wajasiriamali wadogo na
wa kati hapa nchini.
Mwisho
No comments:
Post a Comment