Na Mwandishi wetu, Dar es
Salaam
Mkandarasi mkuu
anaeshughulikia mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es
Salaam, Strabag International ametangaza kufungwa kwa muda kipande cha
barabara ya Mandela hadi makutano ya Ubungo Mataa kuanzia leo.
Akiongea jana na waandishi
wa habari, Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Bw. Yahya Mkumba alisema
kipande cha barabara ya Mandela kuanzia makutano ya barabara ya morogoro upande
wa kushoto uelekeo wa Tabata kuanzia ubungo mataa hadi darajani patafungwa.
Kipande hicho kitafungwa
kuanzia tarehe 25/08/2014 mpaka tarehe 30/08/2014 ili kupisha ujenzi wa kipande
cha barabara hiyo na hivyo kuwalazimu watumiaji wa barabara hiyo kutumia
barabara ya upande mmoja.
Akifafanua zaidi ofisa
uhusiano huyo alisema magari yatakayokuwa yanatokea Mwenge, Kimara na
Shekilango yatalazimika kutumia barabara ya upande wa kulia ambayo pia itakuwa
ikitumika na magari yanayo toka Tabata kuelekea Ubungo.
“Tunaomba radhi kwa
usumbufu utakaotokea,” alisema Bw. Mkumba.
Mradi wa Mabasi yaendayo
haraka unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na kuleta ufanisi wa
usafiri.
Awamu ya kwanza ya mradi
huo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwaka huu.
No comments:
Post a Comment