Mkurugenzi wa Utawala, Raslimali Watu na Mawasiliano wa Wakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Evodius Katare akisisitiza jambo kwa Maofisa
Mawasiliano na Habari kwenye mkutano maalumu uliondaliwa kuwajengea uwezo
maofisa hao ambao Taasisi zao ni wadau wakuu wa mradi huo. Mkutano huo
ulifanyika Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka (DART) umetaka kuwepo kwa ushirikiano miongoni mwa
maofisa habari na mawasiliano wa taasisi zinazoguswa na mradi moja
kwa moja ili kusaidia kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi juu ya
uendeshaji na usimamizi wake.
Mkurugenzi
wa Utawala , Rasilimali Watu na Mawasiliano wa DART, Bw.Evodius R. Katare,
amesema maofisa habari na mawasiliano ni nguzo muhimu katika utoaji wa taarifa
za Mradi na hivyo ili wananchi waweze kuuelewa mradi ni lazima kuwe na
ushirikiano miongoni mwao.
“Sisi
kama DART tunaamini kuwa maofisa habari na mawasiliano wa Taasisi zote
zinazoguswa na mradi huu wakiulewa vizuri mradi huu na kubadilishana taarifa
itasaidia sana kuwaelimisha wananchi na kuwajengea uelewa mkubwa,” alisisitiza
Bw.Katare.
Akizungumza
na maofisa wa habari na mawasiliano kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Usafirishaji
wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),Wizara
ya Ujenzi, Strabag, SMEC, Jiji la Dar es Salaam, Manispaa za Ilala, Kinondoni
na Temeke mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi huyo aliwataka maofisa hao kuwa kitu
kimoja na kukutana kila wakati na kuzumzia maendeleo ya Mradi.
“Nyinyi
ni wadau wakubwa sana wa Mradi na hivyo mnapaswa kujua kila hatua ya maendeleo
ya Mradi ili muweze kuwafamisha wananchi na kwa maana hiyo ni vyema mkaandaa
utaratibu ambao utawawezesha kukutana mara nyingi,” alisisitiza.
Kwa
upande wake Meneja wa Mawasiliano wa SUMATRA, Bw. David Mziray alisema mkutano
utaleta tija katika kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya Mradi kwa wadau kwa kuwa
na sauti moja toka taasisi zote zinazoguswa na huu mradi.
“Mkutano
huu na kukutana kwetu mara kwa mara ni muhimu sana kwetu kwani itatujengea uwezo
na kuuelewa mradi na kuwahabarisha vyema wananchi,” alisema Bw.Mziray na
kuongeza kuwa mradi wa DART utabadilisha kabisa taswira ya jiji la Dar es
Salaam.
Naye msemaji
kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar-es-salaam, Bw. Gaston
Makwembe aliipongeza DART kwa kuandaa mkutano na maofisa habari na
mawasiliano hao na kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na kujengea uwezo
wa kuuelewa mradi.
“Mradi wa
DART umefikia sehemu nzuri na wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wanapaswa
kufahamishwa kila hatua ya maendeleo ya Mradi, matumizi yake na umuhimu wa
kuilinda miundombinu ambayo imeshakamilika,” alisema Bw.Makwembe.
Akichangia
katika mkutano huo, Meneja Mawasiliano wa TANROADS, Bi. Aisha
Malima alisema taarifa sahihi zinahitajika katika mradi wa DART ili
kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii juu ya Mradi pasipo na upotoshaji.
“Taasisi
zetu ni wadau wakubwa katika mradi huu mkubwa wa DART na hivyo ni vyema sisi
wahusika wa mawasiliano tukafanya kazi kwa ukaribu na kuweza kuelimisha jamii
juu ya maendeleo ya mradi,” alisema Bi. Malima.
Mkutano
huo maalumu uliondaliwa na DART na kuhudhuriwa na maafisa
mawasiliano wa taasisi zinazohusika katika Mradi huo kwa lengo la kuwajengea
uwezo na uelewa wa mradi huo kabla ya kukamilika kwa awamu ya kwanza mwishoni
mwa mwaka huu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment