Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu ya
Uwekezaji nchini (EPZA), Dkt. Aldelhem Meru, akisisitiza jambo kwa
waandishi mwishoni mwa wiki kuhusu kongamano la biashara lilofanyika
nchini Marekani hivi karibu na kusema kuwa matunda yameanza kuoneka.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kongamano la maswala ya biashara
lililofanyika nchini Marekani mapema mwezi huu limeanza kuzaa
matunda.
Sasa, wawekezaji kutoka nchi hiyo wameanza
kutaka kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali kwenye maeneo maalumu yaMamlaka ya
Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA).
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo,
Dr. Adelhelm Meru aliwaambia wandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini
Dar es Salaam kuwa kongamano hilo lililojulikana kama “Doing Business in
Tanzania” limeanza kuzaa matunda ya kupata wawekezaji kuwekeza katika maeneo
yake maalumu.
“Katika siku chache baada ya kurejea,
tumepata kampuni tatu ambazo zimeleta maombi ya nia ya moja kwa moja kuwekeza
katika maeneo maalumu,”alisema.
Alisema mamlaka imepokea maombi yanayotaka
kuwekeza katika maeneo ya kuongezwa thamani zao la ngozi, teknolojia ya habari
na mawasiliano (TEHAMA), na ujenzi wa miundombinu katika maeeneo maalumu ya
mamlaka.
Akifafanua zaidi alisema matarajio
yaliyopo kwa sasa ni kuendelea kupata wawekezaji wengi toka nchi hiyo kwa vile
kongamano hilo liliipa nafasi nzuri Tanzania kutangaza fursa zilizopo nchini.
Rais Jakaya Kikwete aliongoza ujumbe wa Tanzania
katika kongamano hilo kubwa.
“Walionesha nia ya kutaka kuwekeza katika
maeneo ya viwanda vya kuongeza thamani mazao ya Kilimo na uzalishaji nishati,”
alifafanua Dk. Meru.
Alitaja maeneo mengine kama utafiti wa
gesi na mafuta, utoaji wa huduma kwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi katika
bahari ya Hindi.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na watu zaidi
ya 400 ambapo kampuni kubwa kutoka majimbo mbalimbali ya nchi humo zilishiriki
ambapo wafanyabiashara wa Tanzania waliweza kukutana na wenzao wa Marekani na
kuzungumza biashara.
“Wengi walitumia fursa hiyo kupata wabia,
kuzungumza na kampuni zinazotoa mikopo na kupata masoko ya bidhaa za
Tanzania,”alisema.
Kongamano hilo lilifanyika baada ya Rais
Kikwete kushiriki mkutano wa Marais wa Afrika na Rais Barack Obama wa Marekani
jijini Washngton D.C.
Kongamano hilo liliandaliwa na EPZA, Kituo
cha Uwekezaji nchini (TIC) na kituo cha uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa
kushirikiana na Corporate Council on Africa ya Marekani.
Mwisho
No comments:
Post a Comment