Na Mwandishi Wetu, Pwani
Serikali imesema inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa
huduma ya maji katika jiji la Dar es Salaam inaimarika na kufikia wananchi
wengi kadiri inavyowezekana.
Viongozi wa Mamlaka ya Maji
Safi na Maji taka Dar-es-salaam (DAWASA) wamesema kuwa wanahakikisha miradi
inayoendelea ya kuimarisha huduma ya maji inakamilika haraka na kwa muda
uliopangwa ili kufanikisha lengo hilo.
Akizungumza na waaandishi
wa habari wakati wa ziara ya kutembelea mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini hivi
karibuni, Mwenyekiti wa bodi ya Dawasa Dkt.Eve Hawa Sinare amesema kwa upande
wa Ruvu Chini upanuzi wa mitambo kwa asilimia 50 utaongeza uwezo wa
kusukuma maji lita milioni 270 kwa siku kutoka pale.
Awali mtambo huo ulikuwa na
uwezo wa kusukuma maji lita milioni 182 kwa siku kwenda katika jiji hilo.
“Ongezeko hili litapelekea
kupungua au kuisha kabisa kwa shida ya maji jijini Dar-es-Salaam na maeneo
jirani,” alisema wakati wa ziara hiyo iliyoshirikisha pia wajumbe wa bodi wa
Mamlaka hiyo.
Alifafanua kuwa ongezekezo
hilo linakwenda sambamba na usambazaji maji hivyo shughuli iliyobaki ni kulaza
mabomba kuelekea Dar-es-Salaam kwa ajili ya usambazaji ambapo zoezi hilo
linaendelea kwa ufanisi mkubwa.
Mwenyekiti huyo aliongezea
kusema kuwa anafurahishwa na kasi ya utendaji na kwamba kuna matarajio kuwa
miradi hiyo itakwisha kwa muda uliopangwa.
“Kama bodi tunajivunia
kuona miradi hii ya maji inakwenda kwa wakati uliopangwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa DAWASA, Mhandisi Archard Mutalemwa alisema mitambo mipya imefungwa
katika vyanzo vya maji vya Ruvu Juu na Ruvu Chini na kuwa hali hiyo itapelekea
upatikaniji mkubwa wa maji jijini Dar-es-Salaam.
Alisema zoezi la ulazaji
mabomba ya kusafirishia maji kutoka Ruvu Juu mpaka Kimara umeshaanza
na unahusisha mabomba matatu yenye kipenyo cha milimita 1200, 1000, na 900.
Aliongezea kuwa kutakuwa na
ukarabati wa matenki ya maji yaliyopo kimara ili kuyafanya kuwa bora zaidi.
Pia Bw. Mutalemwa alielezea
vyanzo vipya za maji vya kimbiji na Mpera na kuwa wameshaanza kuchimba visima
ambavyo vikikamilika vitakuwa vinapeleka maji jijini Dar-es-salaam kwa zaidi ya
lita milioni 260 kwa siku.
“Mara baada ya kukamilika
kwa miradi yote hii mwakani tutakuwa na uhakika wa kupeleka maji jijini kwa
zaidi ya lita milioni 756,000 kwa siku,” alisema Bw. Mutalemwa.
Alisema pamoja na kuwa na
uhakika wa maji safi hapo baadaye kidogo, changamoto iliyopo ni namna ya
kuwafikia wananchi wote jijini, hivyo wahandisi wasanifu wanafanya tathmini ya
usambazaji maji kwa jamii hasa katika maeneo mapya.
Alisema changamoto nyingine
ni namna ya uondoaji wa majitaka jijini kwani kwa sasa ni wananchi alisilimia
10 tu wanaofikiwa.
Wajumbe hao wa bodi
walipanda miti katika maeneo ya mradi waliyotembelea kama kumbukumbu na pia
kutekeleza sera ya serikali katika kutunza mazingira.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment