Monday, August 25, 2014

‘Endless Quest’ kitabu cha insha za theolojia cha zinduliwa

Na Mwandishi Wetu, Musoma

‘Endless Quest’ kitabu kipya chenye mkusanyiko wa insha bora za theolojia zilizotungwa na mtetheolojia maarufu duniani, Padre Profesa Laurenti Magesa kimezitunduliwa rasmi mjini Musoma, Mkoani Mara  hivi karibuni huku wito ukitolewa kwa vijana wa kitanzania kusoma na kuelewa historia ya nchi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa mwishoni mwa wiki, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Idara ya Falsafa (philosophy) na Mafunzo ya Dini, Dkt. Evarist Magoti,ambaye wamehariri kitabu hicho na Profesa Jesse Mugambi, uzinduzi wa kitabu hicho ilikuwa ni sehemu pia ya kuadhimisha miaka 40 ya huduma ya mtheojia padre Magesa.

“Uzinduzi huo ambao ulihudhuriwa na Baba Askofu wa Jimbo la Musoma, Askofu Michael Msonganzila kwenye kuadhimisha sherehe za Padre Profesa Magesa,alishuhudia pia uzinduzi wa kitabu kingine.

Kwa mujibu wa mhadhili huyo,kitabu kingine kilichozinduliwa ni‘What is not Sacred?’ ambacho kimeandikwa na  Profesa Magesa ambaye pia ni Mhadhili katika Chuo cha ‘ Hekima College’ kilichopo  Nairobi nchini Kenya.

“Vitabu hivi viwili vina mambo mengi sana kwa vijana wa kitanzania na wengine wa kiafrika kujifunza kifikra badala kufiria kuwa ni wazungu na kuudharau uafrika ambao ni chimbuko lao,” amesema.

Amesema kuna tabia ambayo imejengenga kwa waafrika wengi kuishi na kujiona kuwa ni wazungu na kubeza mila na tamaduni za kiafrika kabisa.
“Endapo kizazi hiki hakitafundishwa misingi na historia ya tamaduni na mila za kiafrika, basi nina shaka kubwa kitapotea,” alisisitiza Dkt. Magoti.

Akifafanua zaidi kuhusu vitabu hivyo viwili ‘Endless Quest’ na ‘ What is not Sacred?’, Dkt. Magoti alisema vitakuwa vinatumika sana siyo kwenye Taasisi za Elimu ya juu pekee bali pia hata kwa watu wanaopenda kujisomea na kuongeza maarifa.

“Hakuna shaka lolote kuwa vitabu hivi vitasaidia sana kutoa mtazamo au picha ya mwafrika duniani  yaani ‘ African World View’ kwa mtu yeyote atakayesoma,” alisisitiza.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa vitabu hivyo, Askofu Msonganzila, alito changamoto kwa wasomi nchini kutunga vitabu vya aina hiyo kwa lugha ya Kiswahili ili watanzania wengi waweze kupata maarifa yaliyoandikwa kwenye vitabu hivyo.

Aliitaka pia jamii ya kitanzania kuendela kujenga utamaduni wa kujisomea na kujifunza vitu mbalimbali iliwaweze kupanua maarifa na uelewa wao kuhusu dunia.

“Wito wangu kwa watanzania hususani vijana, lazima wajengewe tabia ya kujisomea na kujifunza vitu vingi na vyenye manufaa kwa Taifa letu,” aliongeza Askofu Msonganzila.


Mwisho.

No comments: