Monday, August 18, 2014

Pinda azindua upanuzi wa kiwanda cha Kamal Steels

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji ncnini (EPZA) Dkt. Adelhelm Meru (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Kamal Steels Limited,  Bw. Gagan Gupta muda mfupi mara baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuzindua rasmi upanuzi wa kiwanda hicho, uzinduzi ulifanyaika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Mizengo  Pinda, akinyanyua mkasi juu kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa upanuazi wa kiwanda cha kutengeneza nondo cha Kamal Steels Limited cha jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.Wegine  Mwenyekiti wa kiwanda hicho Bw. Gagan Gupta (katikati ) na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Bw. Said Meck Sadick kushoto.
Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amezindua upanuzi wa Kiwanda cha kutengeza nondo cha Kamal Steels Limited kilichopo jijini Dar es Salaam na kutoa wito kwa viwanda vingine nchini kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Aidha, Waziri Mkuu aliridhishwa na hatua ya upanuzi wa kiwanda hicho na kusema kuwa kitakapo kamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni themanini (80,000,000) za nondo kwa mwaka.

“Nimefurahi kusikia kwamba upanuzi wa kiwanda hiki utakifanya kiwe kikubwa katika nchi za Afrika Mashariki na kuifanya Tanzania kuweza kuzalisha nondo zaidi ya mahitaji yake na ziada kuuzwa nje ya nchi,” alisisitiza Bw. Pinda wakati hafla ya uzinduzi huo mwishoni mwa wiki.

Bw. Pinda amepongeza pia jitihada zinazofanywa na kiwanda cha Kamal Steel hapa nchini ikiwepo upanuzi wa kiwanda hicho cha nondo kwani ukamilikaji wake utachochea zaidi ukuaji wa sekta ya ujenzi.

“Sekta ya viwanda hususan Sekta ndogo ya chuma ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi,” alisema, na kuongeza kuwa mchango wake ni mkubwa sana katika sekta ya ujenzi ambapo bidhaa za chuma zimekuwa zikitoa mchango mkubwa.

Waziri Mkuu pia alichukua nafasi hiyo kuvikumbusha wiwanda vinavyozalisha bidhaa ya chuma hususani nondo kuzingatia ubora wa viwango vya kimataifa vijulikanavyo kama British Standard (BS 460) ili kukidhi mahitaji ya sekta ndogo ya ujenzi wa miradi mbalimbali nchini..

“Sekta ya ujenzi wa miundombinu imekuwa ikikua kwa kasi sasa ili kuwa katika mazingira mazuri ni vyema viwanda vyote vya nondo vikidhi viwango vya kimataifa,”alisema Bw. Pinda.
Alisema baadhi ya miradi mikubwa inayoendelea kujengwa nchini imekuwa ikitumia nondo kutoka nchi jirani kutokana na baadhi ya viwanda vyetu kutokidhi viwango hivi,”alisema

Bw. Pinda aliiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha inaweka kiwango cha chini viwanda kufikia.

Alisema ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya taifa mwaka 2025, sekta ya viwanda hasa sekta ndogo ya chuma ni muhimili katika kufikia malengo hayo.

“Katika miaka ya karibuni, mchango wa sekta hiyio kwa pato la taifa umeongezeka kutoa asilimia 7.8 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 8.3 kwa mwaka 2013,”alisema.

Alisema ukuaji wa sekta hiyo uliongezeka kutoka asilimia 7.8 mwaka 2012 hadi asilimia 8.6 mwaka 2013 na ukuaji huo ulichangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa kama chuma, mabati na saruji.

Naibu waziri wa Viwanda na Biashara,Bi.Janeth Mbene alisema upanuzi wa kiwanda hicho ni matokeo ya mikakati ya wizara yake katika kujenga uchumi thabiti kwa kuzalisha na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini hasa za chuma.

“Kwa sasa viwanda vimeongezeka kutoka vitano mwaka 2005 hadi kufikia 15 na hii inatokana na  upatikanaji wa urahisi wa malighafi,”alisema Bi.Mbene.

Alisema kwa sasa viwanda hivyo vinauwezo wa kuzalisha tani 420,000 za nondo kwa mwaka ambavyo vimewekeza dola za Kimarekani milioni 200.

Alisema mahitaji ya nondo kwa sasa ni tani 300,000 na hiyo inaonyesha kuwa kunauwezo mkubwa wa kuzalisha nondo endapo viwanda vyote vitakuwa vinatumia asilimaia 71 ya uwezo uliowekezwa.
Aidha alisema pamoja na uwezo huo mkubwa bado nchi inaagiza kutoka nje ya nchi wastani wa tani 110,000 za nondo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti  na Mkurugenzi Mtendaji wa Makapuni ya Kamal (Kamal Group) Bw. Gagan Gupta alisema upanuzi wa kiwanda chake unalenga kuongeza uzalishaji zaidi na kuendelea kuwapatia watanzania huduma bora.

“Upanuzi wa kiwanda chetu utaongeza uzalishaji kutoka tani 10,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 80,000 za nodo kwa mwaka,”alisema.

Alisema katika kipindi cha miaka kumi tangu kuanza kwa kiwanda chake kimekuwa ikizalisha nondo zenye viwango vya kimataifa kukidhi mahitaji ya sekta ya ujenzi.


Mwisho.

No comments: