Monday, August 18, 2014

Vitambulisho vya taifa haviwezi kutumika kupiga kura--NEC

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kwa hali ilivyo sasa Watanzania hawawezi kutumia vitambulisho vya uraia kupiga kura, isipokuwa  tu  kadi  zitakazotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC).

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba, amefafanua jana jijini Dar es Salaam kwamba ni makosa kudhani   kuwa vitambulisho vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) vinaweza kutumika kupiga kura.

“Haiwezekani kabisa,” amesisitiza Bw. Mallaba na kuongeza ”tunaomba watu waelewe kuwa kadi za kupiga kura na vitambulisho vya uraia ni vitu viwili tofauti. Vitambulisho vya taifa siyo mbadala wa kadi za kupiga kura.”

Ameeleza kuwa kwa hali ilivyo utoaji wa vitambulisho vya taifa kwa nchi nzima utachukua muda mrefu.  Watu wengi watakuwa hawajapata vitambulisha vya taifa hata baada ya chaguzi zilizoagizwa kisheria kupita.

Mkurugenzi ametoa ufafanuzi huo kufuatia taarifa katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba mtu asiye na kadi  ya kupiga kura anaweza kutumia kitambulisho cha uraia kupiga kura.

Alisema wakati uandikishaji wa NEC unafanyika kwa muda maalum ili kuwahi upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu, uandikishaji wa NIDA hauna muda maalum.

“NEC ina mchakato mfupi wa ukusanyaji wa taarifa za watu wanaoandikishwa na kadi za mpiga kura zinatolewa hapo hapo kituoni baada ya ujazaji wa fomu,” alisema.

Alisema kwa upande wa NIDA, mchakato wa ukusanyaji wa taarifa una utaratibu mrefu kutokana na wahusika zoezi hilo kuwa wengi.

Akielezea zaidi alisema namba ya kadi inayotolewa na NEC ni ya kipekee kwa mtu anayeandikishwa wakati NIDA inaweza kutoa namba zaidi ya moja endapo itabidi kutoa kitambulisho kingine kwa mtu huyo huyo kutokana na kitambulisho cha awali kupotea au kuharibika.

Bw. Mallaba alisema hata kama vitambulisho vya raia vingekuwa tayari, bado tume ingetakiwa kuandaa daftari kwa kuwa vitambulisho vya uraia huwa haviainisha mtu ni mpiga kura wa eneo gani.

“Ukipewa kitambulisho kile utajua huyu ni raia wa Tanzania lakini atakuwa hajaainishwa kwamba huyu ni mpiga kura wa jimbo  fulani  kwa maana ya ubunge au wa kata fulani kwa maana ya udiwani,” alisema.

Alifafanua kuwa  kama wananchi wote wangekuwa na vitambulisho vya taifa, kitu ambacho kingefanyika ni kwa tume kununua kifaa kinachoweza kusoma kitambulisho na kupata taarifa za muhusika na kumpangia muhusika sehemu yake ya kupigia kura.

Alisema swala la kufahamu eneo la wapiga kura na idadi ni la msingi sana katika kufanya maandalizi ya uchaguzi.

“Hata siku ya uchaguzi wenyewe, bila kuelewa kwamba sehemu fulani ina wapiga kura idadi fulani itakuwia vigumu sana kufanya kazi,” alisema.

Alifafanua kuwa hata vyama vya siasa navyo vitapenda hata kabla ya siku ya uchaguzi wafahamu eneo fulani lina wapiga kura wangapi.

“Ni kitu muhimu sana katika demokrasia ya uchaguzi kwa chama kuelewa  katika sehemu fulani kutakuwa na wapiga kura idadi fulani,” alisema, na kuongeza kuwa hata sheria inaitaka NEC siku kadhaa kabla ya uchaguzi kuonyesha idadi ya wapiga kura, majina katika maeneo yao.

Alisema hakuna nchi ya kiafrika inayotumia kitambulisho cha taifa moja kwa moja katika kupiga kura isipokuwa kutumika kurahisisha utaratibu wa kuandaa daftari la kudumu la wapiga kura.

“Kuwa na daftari hakuepukiki,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva alisema uandikishaji wa vitambulisho vya taifa kwa upande mmoja na vitambulisho vya wapiga kura kwa upande mwingine ni shughuli mbili tofauti lakini zinazohusiana kwa karibu na pia zinazohusu wananchi.

“Watanzania wanaokuja mbele ya tume ni wachache kuliko wale wanaoenda kwenye mamlaka inayohusika na vitambulisho vya taifa,” alisema.
Alieleza kuwa zoezi la vitambulisho va uraia litakapokamilika litarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za raia zitakazosaidia matayarisho ya uchaguzi.

“Hakuna mgongano kati ya NIDA na NEC,” alisema.


Mwisho

No comments: