Wednesday, August 6, 2014

Watanzania wahamasishwa kujitolea, uzalendo kupata maendeleo

Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Mercy Sila (katikati) akizungumza na baadhi ya wajumbe waliofanya ziara nchini Korea kujifunza shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kijiji kipya cha maendeleo cha Saemaul Undong hivi karibuni jana wilayani humo.  Kulia ni mlezi wa Umoja huo, Mchungaji Joshua Lee na Mshauri wa umoja huo Bw. Mohamed Dolla.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Mercy Sila (kushoto) akizungumza na wajumbe waliofanya ziara nchini Korea kujifunza shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kijiji kipya cha maendeleo cha Saemaul Undong hivi karibuni jana wilayani Mkuranga.  Kulia ni mlezi wa Umoja huo, Mchungaji Joshua Lee na Mshauri wa umoja huo Bw. Mohamed Dolla.
Mlezi wa umoja wa wajumbe waliofanya ziara nchini Korea kujifunza shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika kijiji kipya cha maendeleo cha Saemaul Undong nchini Korea, Mch. Joshua Lee akizungumza jambo na wajumbe, Mohamed Dolla (kushoto) na Mwajuma Kingwande (katikati) walipotembelea eneo ambapo patajengwa daraja kwa nguvu za wananchi wakishirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga ili kutatua tatizo la mawasiliano kati ya kijiji cha Njia Nne na Nyamihimbo.
Na Mwandishi wetu, Mkuranga

Kujitolea na uzalendo kwa nchi vimetajwa kama nyenzo muhimu za maendeleo kwa taifa la Tanzania.

Ushauri huo umetolewa na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Bi. Mercy Sila aliyekuwa anaongea na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika uchaguzi wa viongozi wa wajumbe waliotembelea kijiji cha maendeleo cha mfano cha Saemaul Undong nchini Korea ya Kusini hivi karibuni.

Bi. Sila alisema watanzania wakiamua wanaweza kuendelea na ndio msingi mkubwa wa kuleta maendeleo popote pale, hasa watu wanapohamasishwa kufanya kazi kwa umoja nguvu na msihikamano wa kweli.

“Suala la kimaendeleo si la viongozi bali ni wananchi wenyewe,” alisema Bi Sila.

Aliongeza kuwa Wakorea wamefanikiwa na kupiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na nidhamu ya hali ya juu katika kufanya kazi kwa kujitolea hivyo ni jukumu la viongozi kutoa hamasa kwa wananchi kulijua hilo.

“Tumeenda Korea tumeona wenzetu waklivyo kuambali, maendeleo yao yametokana na wananchi kupewa hamasa na kuona nchi ni ya kwao na si mtu kutoka nje” aliongeza

Alisisitiza kuwa umoja waliouwanzisha katika wilaya ya Mkuranga unapaswa kuwa wa kitaifa kwani ni jambo kubwa na la msingi kuona vijiji vinakua kimaendeleo hasa kwa wananchi wenyewe kuweka nguvu zao mbele.

“Wananchi wa kawaida Korea hawahitaji fedha kwanza, wamefundishwa namna ya kujitolea kujenga Taifa lao,”alisisitiza.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema vijiji vya Mfulu Mwambao pamoja na Njia Nne ndio vimefanywa vijiji vya mfano katika harakati hizo za kuleta maendeleo ya kweli na hilo limetokana na baadhi yao kwenda nchini Korea kujifunza namna watu wanavyofanya kazi kwa kujitolea.

“Wananchi wangu katika vijiji hivyo wameanza kuelewa na hii ni kutokana na baadhi yao kwenda korea kujifunza,” alisema.

Wananchi hao walienda katika moja ya maeneo ya mfano nchini humo na kijionea jinsi watu walivyojitolea katika kufanya kazi na kujenga nchi yao.

“kutokana na hali hiyo huu umoja wetu wa huku tulionzisha tutauita Saemaul Undong Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake, mlezi wa umoja huo,  Saemaul Undong, Mchungaji Joshua Lee alisema watanzania ni watu wenye utajiri mkubwa hivyo wanatakiwa kuhamasishwa ili kuweza kupata matunda zaidi ya utajiri huo.

“hakuna ambacho hakipo hapa, ni watu kuhamasishwa kufanya kazi ili wawe na maono ya mbali,” alisema.

Aliongeza kuwa huu ni wakati wa watanzania kuweka uzalendo mbele, kufanya kazi kwa kujitolea zaidi pasipo kudai fedha mara kwa mara na kwa kufanya hivyo wanaweza kuwa kama wakorea katika miaka ijayo.

Katika Uchaguzi huo wa umoja wa wajumbe waliotembelea nchini Korea uliwachagua Mkuu wa Wilaya Mstaafu wa Wilaya ya Mkuranga Bw. Henry Clemens kuwa Mwenyekiti, Bw. Gaudence Kayombo kuwa makamu Mwenyekiti, Apolinary Rutaga katibu na Mwajuma Kingwande kuwa mweka hazina huku Bw. Mohamed Dolla akiwa mshauri wa umoja huo.


Mwisho  

No comments: