Monday, July 28, 2014

Serikali, sekta binafsi wakaribisha uhusiano wa vyuo vya Mzumbe, Stellenbosch

Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Prof. Adolph Mkenda (kulia) akiwa pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Fedha na Utawala, Prof. Faustin Kamuzora na Afisa Mkuu Mtendaji wa Kitengo kinachotoa mafunzo ya menejimenti katika shule ya biashara ya Chuo Kikuu cha Stellenbosch, Prof. Frik Landman (katikati) mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Chuo Kikuu Mzumbe kimefikia makubaliano na Chuo hicho ambapo kozi mbalimbali zitakuwa zinatolewa katika kampasi ya chuo hicho Dar es Salaam kuanzia mwezi wa Nane mwaka huu.
Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Prof. Adolph Mkenda (kushoto) akiwa pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Fedha na Utawala, Prof. Faustin Kamuzora mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Chuo Kikuu Mzumbe kimefikia makubaliano na Chuo hicho ambapo kozi mbalimbali zitakuwa zinatolewa katika kampasi ya chuo hicho Dar es Salaam kuanzia mwezi wa Nane mwaka huu.  Prof. Mkenda ndie aliyezindua ushirikiano kati ya vyuo hivyo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Serikali na sekta binafsi nchini zimesifu ushirikiano mpya wa kitaaluma uliozinduliwa kati ya vyuo vikuu vya Mzumbe na shule ya biashara ya chuo kikuu cha Stellenbosch cha Afrika ya Kusini.

Chuo Kikuu Mzumbe kimeingia makubaliano na Chuo hicho kwa nia ya kutoa mafunzo ya menejimenti kwa maafisa wa serikali na sekta binafsi hapa nchini na Afrika ya Mashariki kwa ujumla.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa programu hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba alisema ushirikiano huo ni hatua nyingine ya maendeleo kwa taifa.

Naibu Waziri huyo aliyewakilishwa na Naibu katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Adolph Mkenda alisema serikali inakaribisha ushirikiano huo ambao alisema unaendana na mkakati wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa.

“Watanzania watafaidika na mpango huu ambao masomo yake yatakuwa yanatayarishwa na wataalamu toka vyuo hivi viwili,” alisema, na kuongeza kuwa serikali ingependa kuona ushirikiano kama huu zaidi hapa nchini.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni, Dk. Elisante Gabriel alisema ushirikiano huo umekuja wakati muafaka.

“Nawatakatia mafanikio na ninashauri kampuni hapa nchini kupeleka maafisa wake kusoma programu hizo zitakazokuwa zinatolewa Mzumbe,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alikaribisha uhusiano huo na kusema kuwa wadau wa sekta wanahitaji mafunzo kama hayo.

“Viongozi katika sekta binafsi wanatakiwa kuwa washindani na program hii inatoa fursa pekee kufanikisha hilo,” alisema.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kitengo kinachotoa mafunzo hayo katika Chuo Kikuu cha Stellenbosch, Prof. Frik Landman alisema kama sekta binafsi na serikali wataona umuhimu, uhusiano huo utakuwa chachu ya maendeleo ya Tanzania.

“Tunafuraha kuwa tunaweza kutoa mchango wetu kupitia njia hii,” alisema.

Alisema kuwa ni muhimu na kitu cha thamani kwa taasisi katika nchi zikawa na mameneja wenye ufanisi ili kuweza kuzalisha na kuleta tofauti.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Fedha na Utawala, Prof. Faustin Kamuzora alisema kuwa uhusiano huo unatokana na mpango mkakati wa chuo hicho unaolenga kushirikiana na taasisi toka sekta za umma na binafsi.

Alisema kuwa kuendeleza raslimali watu katika taasisi au kampuni yoyote ile ni jambo la msingi.

“Hii ni nafasi muhimu kwa taasisi hapa nchini,” alisema.

Kwa mujibu wa mratibu wa mafunzo hayo hapa nchini, Prof. Shiv Tripathi awamu ya kwanza ya mafunzo hayo itatolewa hapa jijini katika chuo hicho kuanzia tarehe 28-29 Agosti mwaka huu.

Prof. Tripathi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Kozi fupi na Ushauri katika chuo hicho alisema mafunzo hayo yatatolewa na msomi maarufu duniani, Dr. John Westwood aliyekuwa katika shule ya biashara ya Manchester lakini sasa anaishi Afrika ya Kusini.

Mwisho


No comments: