Tuesday, July 8, 2014

TTCL yatoa msaada, yahimiza wengine kufanya hivyo

Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu nchini (TTCL), Bw. Amin Mbaga (kulia) akimkabidhi msaada wa bati 100 Mwenyekiti wa kituo cha kulelea watoto yatima na waishio mazingira magumu cha Female Youth Help Age Trustee, Bw. Simon Mganga (wa tatu kushoto) kwa ajili ya kuezekea bwalo la shule ya awali ya watoto hao mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.  Mwenye shati ya bluu ni ni Mkuu wa Kituo hicho, Bw. Ibrahim Daniel na mlezi wa watoto, Bi. Mwanaidi Hamisi (kushoto).
Na Mwandishi wetu, Pwani
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imeendelea kutoa misaada katika vituo vya watu wasiojiweza na kuhimiza wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kusaidia zaidi wenye mahitaji katika jamii.

Kampuni hiyo mwishoni mwa wiki imetoa msaada wa mabati 100 yenye thamani ya Tshs milioni 1.7 kwa kituo cha watoto yatima Female Youth Help Age Trustee kilichopo Pangani, Kibaha mkoani Pwani.

Msaada huo umetolewa ili kukarabati bwalo la kituo hicho ambalo liliharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha miezi michache iliyopita.

“Tuna imani msaada huu utasaidia kukarabati bwalo hili ambalo ni muhimu kwa maisha ya watoto hawa,” alisema Meneja Uhusiano wa TTCL, Bw. Amini Mbaga wakati wa kutoa msaada huo.

Alisema kuwa kampuni hiyo inawajibu wa kutoa msaada katika jamii, hasa wale wasojiweza kwa kuwapatia mahitaji ya msingi kama elimu na chakula bora.

“Tumeona kwamba tujikite katika maswala ya elimu na afya,” alisema Bw. Mbaga.

Alisisitiza kuwa kuna umuhimu kwa wadau wengine kuendelea kusaidia vifaa na dawa, vifaa vya mashuleni kama madawati na vitabu, chakula miongoni mwa vingine kama mahitaji ya msingi ya binadamu.

“Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia serikali kufikia malengo yake ya maendeleo kwa haraka zaidi,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa kituo hicho, Bw. Simon Mganga alitoa shukrani katika kwa kampuni hiyo na kusema msaada huo utawasaidia sana.
Alifafanua kuwa kituo hicho kina jumla ya watoto 350 ambao wapo katika vituo tofauti vya kulelea watoto wasiojiweza.

Alisema kuwa bado wanahitaji simenti, mchanga, kokoto  kwa ajili ya ujenzi, maji, na umeme kwa ajili ya kuboresha kituo hicho.

Akielezea kituo cha Kibaha, Mkuu wa kituo hicho, Bw.Ibrahim Daniel alisema wana watoto 30 ambapo 14 ni wa kiume na 16 ni wa kike.

“Tuna lengo la kutoa elimu ili watoto wafikie ngazi ya juu ila kwa sasa tumeanza na elimu ya awali,” alisema.

Kituo hicho kina madarasa nane; ofisi mbili; bwalo moja na bweni moja katika eneo la ukubwa wa hekta 15.

Mwisho.

No comments: