Wednesday, July 2, 2014

Tanzania yaongoza Afrika Mashariki kuvutia mitaji ya nje ya uwekezaji

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Katika kile kinachoonekana kama matokeo ya juhudi za kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji, Tanzania sasa inaongoza kama nchi yenye mitaji mikubwa ya uwekezaji toka nje katika Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Biashara na Maendeleo (UNCTAD), mwaka 2013, Tanzania ilikuwa na mitaji toka nje yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 12.7 ikiipita Kenya iliyokuwa na dola bilioni 3.4 na Uganda dola bilioni 8.8.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kwa mwaka 2013 pekee Tanzania ilivutia mitaji ya uwekezaji toka nje yenye thamani ya dola bilioni 1.9 na kuipita mbali Kenya iliyovutia dola milioni 514 katika kipindi hicho.

Akiongelea kuhusu takwimu hizo mpya, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bi. Juliet Kairuki alisema ni jambo la kujivunia.
“Nadhani Tanzania ina haki ya kujisifu...si kazi ndogo,” alisema.

Alieleza kuwa takwimu hizo ni kielelezo cha juhudi za serikali kuweka sera nzuri za uwekezaji na hatua mbalimbali inazofanya kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na biashara yanakuwa mazuri.

“Viongozi wetu, ikiwepo Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inahusika na uwekezaji, wamefanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kivutio cha uwekezaji, na haya ndio matunda yake,” alisema.

Alisema kuwa katika juhudi hizo serikali imeweka vivutio mbalimbali vya uwekezaji ambavyo vinarahisisha biashara na uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje.

“TIC inaamini kuwa kuongezeka kwa uwekezaji kutaleta ustawi wa maisha kwa watanzania kwa kuzalisha ajira mpya, kuongeza mapato na kuleta teknolojia na ujuzi mpya,” alisema.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Bi. Kairuki alitoa angalizo akisema kuwa pamoja na kwamba Tanzania imevutia mitaji mikubwa bado kazi kubwa inatakiwa kufanyika ili kushawishi kampuni kubwa za kimataifa kujenga miradi mikubwa kama viwanda hapa hapa nchini.

“Alisema uwekezaji wa aina hiyo ni wa muhimu kwa taifa kwani ni uwekezaji wa muda mrefu,” alisema.

Alifafanua kuwa bado kazi kubwa inatakiwa kufanyika ili kubuni fursa mpya za uwekezaji ili kuvutia zaidi mitaji.

TIC iliundwa mwaka 1997 kwa dhumuni la kuratibu, kuvutia na kusaidia uwekezaji nchini na kushauri serikali kuhusiana na maswala ya sera za uwekezaji.

Chombo hicho kinahusika na uwekezaji wenye kiwango cha chini cha mtaji cha dola 300,000 kwa wawekezaji wa nje na dola 100,000 kwa wawekezaji wa ndani.

Mwisho


No comments: