Monday, July 21, 2014

Ole Naiko achagiza taasisi, watu binafsi kusaidia zaidi wenye mahitaji

Mlezi wa Diana Women Empowerment Organisation (DIWEO) ambae pia ni Balozi wa heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emmanuel Ole Naiko (wa pili kushoto) akisalimiana na mmoja wa wawakilishi wa Taasisi ya Kimataifa kutoka nchini Marekani inayoshughulikia masuala ya elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu (IASE), Ms. Meghan Gallagher (kulia) wakati ujumbe huo ulipotembelea nchini kuangalia maendeleo ya vituo vilivyo chini ya DIWEO hapa nchini mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  katikati ni Dr. Iris Drower kutoka  IASE, na Bi. Mary Gale pia wa taasisi hiyo (kushoto) na Bi. Swaleha Mohamedali (wa pili kulia).
Mlezi wa Diana Women Empowerment Organisation ( DIWEO) ambae pia ni Balozi wa heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emmanuel Ole Naiko (kushoto) akifurahia jambo na  Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa kutoka nchini Marekani inayoshughulikia masuala ya elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu (IASE), Bi. Mary Gale (kulia) mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Ujumbe wa taasisi hiyo uko nchini kuangalia maendeleo ya vituo vilivyo chini ya DIWEO.  Katikati ni Mwenyekiti wa DIWEO, Bi. Farida Khakoo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi, Mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi na watu binafsi wametakiwa kuzidi kutoa mchango wao kusaidia kusomesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Wito huo umetolewa na Mlezi wa Diana Women Empowerment Organisation (DIWEO) Bw. Emmanuel Ole Naiko jijini Dar es Salaam jana alipokutana na viongozi wa Taasisi ya Kimataifa kutoka nchini Marekani inayoshughulikia masuala ya elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu International Association of Special Education (IASE) katika nchi za Amerika ya Kusini, Afrika na Asia.

Bw. Ole Naiko ambaye pia ni balozi wa heshima wa Botswana nchini Tanzania alisema umefika wakati taasisi na mashirika mbalimbali kuzidi kuwasaidia watoto hao ili waweze kuishi kama jamii nyingine za kitanzania na kuondokana na dhana kuwa wametengwa.

“Watoto hawa wanahitaji msaada kutoka kwetu,” alisema balozi Ole Naiko.

Akiongelea taasisi hiyo alisema kuwa inachofanya ni kuangalia na kuhakikisha kuwa misaada wanayotoa inawafikia walengwa na inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

“Kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana ya kujitoa katika nchi zetu hizi, ni vema wakaungwa mkono na taasisi pamoja na mashirika mengine,” aliongeza balozi huyo.

Alisisitiza kuwa moja ya sifa kubwa Tanzania iliyonayo ni kutumia misada inayoletwa na wahisani kama hao na kutumika kwa matumizi sahihi na kwa wakati.

 “Sifa kubwa tuliyonayo ni kufikisha misaada hii sehemu zinazohusika kwa wakati na kwa matumizi yaliyokusudiwa” alisisitiza.

Taasisi hiyo inayofanya kazi katika nchi za Bangladesh, Colombia, India, Malawi, Tanzania na Vietnam, ilianzanishwa mwaka 2005 huku ikijikita zaidi katika elimu na afya hasa kwa nchi zinazoendelea kiuchumi Duniani.

Kwa upande wake, mmoja wa wawakilishi wa taasisi hiyo ya kimataifa, Bi. Mary Gale alisema DIWEO ni taasisi ya kuigwa hapa nchini kutokana na juhudi zake za kusadia watu wanaoishi katika mazingira magumu.

“Napenda kuipongeza DIWEO kwa juhudi zake na hasa mwenyekiti mama Farida Khakoo” alisema Bi. Gale.

Alisema hawatasita kusaidia jamii ya watu wanaoishi katika mazingira magumu pindi wanapoambiwa, kwani hilo ni jukumu lao na wanapaswa kujitoa kwa namna yoyote ile.

“Tumedhamiria kuwaokoa watu wa aina hii hasa watoto kupitia elimu, ni lazima tutekeleze kile tulichokusudia,” aliongeza.

Alisistiza kuwa, watu wanaoishi katika mazingira magumu hawakupenda hivyo ni jukumu la watu walio na uwezo kuwajali  wengine kwa moyo.

Ujumbe wa taasisi hiyo uko nchini  kuangalia maendeleo katika baadhi ya  vituo vilivyo chini ya taasisi ya DIWEO na kuzungumza na kuwafariji watu wanaoishi katika mazingira magumu.


Mwisho

No comments: