Wednesday, July 9, 2014

Serikali imejipanga kupambana dawa za kulevya—Lukuvi

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imejipanga vyema kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya na itakabiliana na wahusika kwa kutumia kila mbinu kufanikisha vita hiyo.

Mbinu hizo zinahusisha pamoja na nyingine kurekebisha sheria na miongozo ya mapambano na dawa za kulevya na pia kutoa adhabu kali na haraka kwa wale wanaobainika kuhusika na biashara hiyo haramu.

Akizungumza hivi karibuni kuhusu maadhimisho ya siku ya kupiga dawa za kulevya Duniani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Bw. William Lukuvi alisema juhudi kubwa zitaelekezwa katika kuzuia biashara hiyo hapa nchini kwa kuanzishwa mikakati ya ufuatiliaji na kuunda chombo chenye nguvu zaidi katika kupambana na tatizo hilo.

“Ninatoa wito kwa wananchi na wadau wengine wote kuendelea kushirikiana na serikali katika kupiga vita dawa za kulevya,” alisema.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye tatizo kubwa la dawa za kulevya kulingana na takwimu za ukamataji wa dawa hizo.

Katika kipindi cha Januari 2014 hadi Juni 2014 jumla ya kilo 220 za heroin zikihusisha watuhumiwa 18 na kiasi cha kilo 15.4 za cocaine zilikamatwa na watuhumiwa 7 walihusika.

Pia alisema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza tatizo la usafirishaji haramu wa kemikali bashirifu kama ephedrine ambazo hutumika kutengeneza dawa za kulevya.

Alisema kuwa dawa za kulevya ni tishio kwa maendeleo ya taifa kwa sababu matumizi ya dawa hizo hupunguza tija na ufanisi wa nguvu kazi ya taifa; kuzorotesha afya za watumiaji na kuwa chanzo kikubwa cha uhalifu kijamii na kiuchumi.

“Matumizi ya dawa hizi yanahusishwa sana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi, homa ya mapafu, moyo na kifua kikuu,” alisema.

Hapa nchini, vijana ni kundi kubwa linaloendelea kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya.  Pia vijana wamekuwa wakitumiwa zaidi kufanya au kuwezesha biashara ya dawa za kulevya.

Kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa “Uteja wa dawa za kulevya unazuilika na kutibika, Chukua hatua.”

Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya Tanzania ilianzishwa kwa Sheria ya Kuzuia Biashara ya Dawa za Kulevya, Na. 9 ya mwaka 1995 Sura ya 95.

Sheria hii inaharamisha/kukataza uzalishaji (kilimo na utengenezaji), usafirishaji, uuzaji, uhifadhi, usambazaji, utumiaji na ufadhili au kusaidia shughuli yoyote inayowezesha upatikanaji wa dawa za kulevya nchini pamoja na kutoa adhabu kwa makosa hayo.

Kadhalika, sheria hii imeweka utaratibu wa kuzuia uchepushwaji wa dawa za tiba zenye madhara ya kulevya ili zitumike kwa ajili ya tiba pekee.


Mwisho

No comments: