Wednesday, July 9, 2014

Prof. Maghembe awataka wazazi Mwanga kushirikiana na walimu

Mkuu wa shule ya Sekondari Kisangara Mwalimu Omary Mbelenji wa kwanza kushoto akimsikiliza Waziri wa Maji ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe, wa kwanza kulia, wakati alipofanya ziara Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro hivi karibuni ya  kutembelea shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinazofanywa  jimboni humo, katikati ni mwenyekiti wa Bodi wa Shule ya Sekondari Kisangara Bw. Selemani Said Mrutu.
Waziri wa Maji ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe, watatu kutoka kulia akiangalia moja ya vifaa vilivyofungwa katika maabara ya Shule ya Sekondari Mgagao wakati alipofanya ziara Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro hivi karibuni ya  kutembelea shughuli mbalimbali za kimaendeleo jimboni humo, kulia ni Mkuu wa Shule hiyo Mwali Onesmo Mfangh, wengine katika picha ni Mwenyekiti wa ccm kata ya Mgagao Mh. Shabani Ngalevo na wa pili kulia ni  Diwani kata ya Mgagao Bw. Eliezer Mkumbwa.
Na Mwandishi Wetu, Mwanga

Wazazi waliopo katika kijiji cha Kriya Kilichopo katika Kata hiyo Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutoa ushirikiano kwa walimu ili watoto waliopo katika shule ya sekondari Kriya waweze kuwa na ufaulu mzuri kuliko ilivyo sasa.

Akizungumza na watendaji katika kata za Kriya, Lembeni na Mwanga Waziri wa Maji ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe alisema maendeleo ya kiuchumi katika nchi na mahali popote pale hayawezi kupatikana kama watu wake watakua hawana elimu.

Waziri Maghembe alikuwa ziarani katika wilaya ya Mwanga kutembelea shughuli mbalimbali za maendeleo jimboni humo hivi karibuni.

“Wajibu mkubwa mlionao wazazi ni kusimamia watoto hawa, ni lazima mshirikiane na walimu hawa watoto wasome,”alisema Profesa Maghembe.

Alisema serikali imejenga shule ili kupunguza matatizo ya watoto kukosa elimu, na kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo, hivyo ni jukumu la wazazi kusimamia na kuhimiza wazazi pamoja na walimu kutoa elimu bora kwa watoto.

“Elimu ni hatua kubwa kuelekea katika maendeleo, ni lazima bodi ya shule hii isimame imara kufuatilia jambo hili,”alisema.

Aliongeza kuwa pamoja na kuongezeka kwa walimu kutoka wanne hadi walimu wapatao 13 hivi sasa, shule imeendelea kutofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne.

“Sitaki jambo hili lijirudie, watoto watatu wanakwenda kidato cha sita wakati shule nyingine zinatoa watoto 18 hadi 20, wazazi hapa lazima mbadilike,” alisisitiza.

Alisema sekta ya elimu katika wilaya ya Mwanga ndio mkombozi pekee kwa vizazi vijavyo, hivyo ni jukumu la wananchi wote kuwahimiza watoto na kuacha kuwaonea haya kuwaambia pale wanapokosea kwa sababu hayo ndio maisha yao.

“Sioni sababu ya mzazi kumuogopa mtoto wake, mtoto umemzaa mwenyewe kwanini akushinde, hatuwezi kulea watoto kilegelege hivi,” alisema.

Alisema nidhamu mbovu ndio inayochangia watoto kutofanya vizuri katika masomo huku akiongeza kuwa watoto wamekuwa wakishinda vijiweni badala ya kujisomea pindi wanaporudi nyumbani.

“Suala la mzazi kumuacha mtoto anazurura hovyo badala ya kujisomea naomba liachwe mara moja litawagharimu watoto wenu kwa kiasi kikubwa, ”aliongeza Waziri Maghembe.

“Naomba sana wazazi hawa watoto wenye simu hasa watoto wa kike, jaribu kumuliza mwanao ni nani amemnunulia simu, hili jambo ni hatari sana chunguzeni hao watoto wenu” alisisitiza.

Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia watoto kujifunza yale waliofundishwa shuleni na hivyo kupunguza baadhi ya wanafunzi wanaotoka shuleni na kupitia sehemu ambazo ni hatarishi kwa maisha yao.
      
Mwisho





No comments: