Mwenyekiti wa kamati maalum ya Wizara ya Maji, Eng. Hamis Blangson (kulia) akisikiliza jambo wakati wa operesheni maalum ya kupambana na watu wanaojiunganishia maji kinyume na sheria na kusababisha hasara kwa serikali na matatizo ya huduma hiyo kwa wananchi. Zoezi hilo limefanyika jana katika eneo la Kwa Msuguri, Kimara jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni wajumbe wa kamati hiyo, Bw. Twaha Mohamed (kushoto) na Bw. Juma Maingu (katikati). Zoezi hilo linaendelea.
Kifaa cha kubebea vifaa vizito cha DAWASA kikiondoka na moja
ya mashine ya kutengenezea kutengenezea matofali katika eneo la Kwa Msuguri,
Kimara jijini Dar es Salaam jana. Wizara
ya Maji iliamrisha kukamatwa kwa vifaa na mali mbalimbali za Martin Kessy
aliyekuwa amejiunganishia maji kinyume na sheria na kufanya biashara ya
kufyatua matofali. Zoezi hilo
linaendelea.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imezidi kuimarisha mapambano dhidi ya watu wanatumia
maji bila kufuata taratibu na sheria na hivyoi kusababisha upungufu wa maji kwa
watumiaji wengine na hasara kubwa ya mapato.
Katika juhudi za hivi karibuni kabisa, Wizara ya Maji kwa
kushirikiana na DAWASA na DAWASCO, zimeendesha zoezi maalum katika eneo la Kwa
Msuguri, Kimara jijini Dar es Salaam ambapo vifaa na mali mbalimbali
zimekamatwa.
Katika operesheni hiyo, wajumbe wa kamati maalum iliyoundwa
na Wazara hiyo ilikamata mashine mbalimbali na vifaa vya kufyatulia matofali, maelfu
ya matofali mali ya Martin Kessy ambae awali alikuwa amepewa onyo na serikali
kusitisha shughuli hiyo ambayo alikuwa anaifanya kwa kujiunganishia maji isivyo
halali.
Mwenyekiti wa kamati hiyo maalum ya Wizara, Eng. Hamis
Blangson aliwaambia waandishi wa habari katika eneo la tukio kuwa uamuzi huo
umetekelezwa kufuatia amri ya mamlaka za juu za Wizara ya Maji.
“Tunafanya hivi kuonyesha kuwa serikali inamaanisha inapotoa
maelekezo,” alisema, na kuongeza kuwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa
dhidi ya Kessy.
Alisema katika eneo hilo, Kessy alikuwa amejiunganishia bomba
la maji kinyume na sheria na kupoteza lita 5,000 kwa dakika au sawa na lita 300,000
kwa saa au lita milioni 7.2 kwa siku.
“Kiwango hiki ni sawa na upotevu wa karibu Tshs bilioni 8 kwa
saa kwa viwango vya sasa,” alisema.
Kessy amefanya shughuli hiyo kwa karibu miaka 10 katika eneo
hilo.
Alisema tatizo la kujiunganishia maji kiholela limekuwa sugu
kwa mikoa ya Pwani na Dar es Salaam na kuwa sasa serikali imeamua kulimaliza.
Afisa huyo wa Wizara alifafanua kuwa kukomeshwa kwa kero hiyo
kutasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza tatizo la maji katika maeneo ya mikoa
hiyo ambayo alisema kuna wafanyabiashara wakubwa wa matofali na wengine
takribani 40 waliojiunganishia maji kinyemela.
“Watu hawa wanasababisha hasara kubwa sana kwa serikali na upotevu
mkubwa wa maji,” alisema, na kuongeza kuwa hali hiyo haikubaliki.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara hao kwenda kwa mamlaka husika
ili waambiwe taratibu maalum za kufuata ili kuepukana na mkono wa sheria.
Pia alitoa wito kwa wananchi kuzidi kutoa taarifa za watu
wasiowaaminifu wanaojiunganishia maji bila kufuata taratibu na kusababisha
shida ya maji.
“Tunapokea malalamiko yoyote kuhusiana na wahalifu kama
hawa…wananchi waje na tutazishughulikia,” alisema.
Kamati hiyo maalumu ni moja ya kamati za kikundi kazi
kilichoundwa na Wizara mwezi Februari mwaka jana kuhakikisha kuwa kero na
matatizo mbalimbali ya maji yanatatuliwa na kurahisisha upatikanaji wa maji kwa
wananchi.
Kwa mujibu wa afisa huyo, zoezi hilo ni endelevu hadi hapo
serikali itakapojiridhisha kuwa kero hiyo imekwisha.
Serikali inatekeleza miradi mbalimbali kuhakikisha kuwa jiji
la Dar es Salaam na miji mingine nchini inapata maji safi, salama na ya
uhakika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment