Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mtandao wa Taasisi za Wakurugenzi Afrika (ACGN)
umezidi kukua kwa kupata wajumbe wapya wawili katika mkutano wake jijini Dar es
Salaam.
Wajumbe waliosaini makubaliano na mtandao huo ni
taasisi ya wakurugenzi toka Tunisia na Kituo cha Utawala Bora cha Misri.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika mkutano wa mtandao
huo uliomalizika jijini hivi karibuni.
Kituo cha Utawala Bora wa Mashirika Taasisi ya
wakurugenzi Ethiopia nayo iko katika mchakato wa kujiunga na ilihudhuria
mkutano huo kama mtazamaji tu.
Pia mtandao huo ulifikia makubaliano ya ushirikiano na
Taasisi ya Maadili ya Afrika ya Kusini pamoja na taasisi ya kimataifa ya
uhasibu, ACCA.
“Tunazidi kukua lakini bado kazi ni kubwa...tunahitaji
wanachama wengine zaidi,” Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wakurugenzi
Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa ACGN, Bw. Said Kambi aliwaambia waandishi wa
habari mwishoni mwa mkutano huo.
Mtandao huo ulianzishwa mwezi Oktoba mwaka jana.
Kwa sasa mtandao huo una wanachama taasisi toka nchi
13 na washirika wengine saba.
Alisema ushirikiano na taasisi ya maadili ya Afrika ya
Kusini utasaidia kuimarisha maadili katika uendeshaji wa mashirika barani
Afrika wakati ushirika na ACCA utasaidia kutoa mafunzo ya kitaalam, utafiti na
kubadilishana taarifa.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wakurugenzi Kenya,
Bw. Meshack Jerome alisema utawala bora wa mashirika ni kitu muhimu kwa
maendeleo ya nchi za Afrika ya Mashariki.
Alizitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuhakikisha
zinazingatia uongozi bora wa mashirika ili kufikia maendeleo endelevu.
“Taasisi hii iliyoanza mwaka 2004 imesaidia kwa
kiwango kikubwa nchi yetu kupambana na ufisadi na kuimarisha maadili katika
nchi yetu,” alisema.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa taasisi hiyo
ya maadili Afrika ya Kusini, Prof. Deon Rossouw alisema utawala bora wa
mashirika unahusu kuendesha mashirika kwa mafanikio na kwa uwazi.
“Nina furaha kuwa moja ya wadau wamtandao huu,”
alisema.
Awali akiongea katika mkutano huo, Mwenyekiti wa ACGN,
Bi. Jane Valls alizishauri serikali za Afrika na Tanzania kufikiria kuwa na
muongozo thabiti utakaoweka viwango, na maadili yatakayopaswa kufuatwa na
mashirika.
Bi. Valls ambae pia ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi
ya Wakurugenzi Mauritius (MIoD) alisema kuwa uendeshaji wa mashirika na
makampuni ni jambo la muhimu sana kwa maendeleo endelevu ya nchi yoyote.
“Unaweza kuliangalia swala hili katika kiwango cha
mashirika au nchi,” alisema.
Alisema kuwa uendeshaji bora wa mashirika barani
Afrika ni muhimu sana kwa sasa ambapo biashara miongoni mwa mataifa ya Afrika
inakuwa na pia mitaji ya uwekezaji barani humo inazidi kuongezeka.
“Imeonekena kuna umuhimu wa kuwa na mikakati ya
kutengeneza miongozo ya uendeshaji mashirika ili kuchochea biashara na kuwa na
viwango vya kimataifa barani Afrika,” alisema.
Waanzilishi wa mtandao huo walikuwa ni Taasisi za
Wakurugenzi toka nchi za Kenya, Malawi, Mauritius, Morocco, Msumbiji, Afrika ya
Kusini na Tanzania.
Wengine ni taasisi toka Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Mtandao huu unalenga kujenga uwezo wa taasisi
wanachama na kuendeleza uendeshaji bora wa mashirika katika sekta binafsi na
umma barani Afrika.
ACGN iliundwa kujenga uwezo wa wanachama wake
kuimarisha uendeshaji wa mashirika, na kujenga mashirika bora barani Afrika
miongoni mwa mambo mengine.
Mtandao huo pia unatoa fursa kwa watunga sera na wadau
wengine kujadiliana kuhusiana na maswala mbalimbali yanayohusiana changamoto
mbalimbali zinazohusiana na uendeshaji wa mashirika na kampuni barani Afrika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment