Rais Jakaya Kikwete akiangalia baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na moja ya kiwanda kilichowekeza katika eneo la Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA) wakati alipotembelea banda la mamlaka hiyo katika maonyesho ya 38 ya Biashara ya Kimataiafa ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto ni Mkurungenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru na mwakilishi kampuni ya Fresh Air LTD, Bw. Bernard Harrison (kulia).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalum wa
Uwekezaji (EPZA), Dk. Adelhelm Meru (kulia), akimueleza jambo Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani (katikati) wakati Waziri huyo alipotembelea
banda la mamlaka hiyo katika maonyesho
ya 38 ya Biashara ya Kimataiafa ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Watanzania wametakiwa kujivunia mafanikio yanayoendelea kujitokeza
katika maeneo maalumu ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) na
kuchangamkia fursa za uwekezaji katika maeneo hayo.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Titus Kamani alitoa
ushauri huo wakati alipotembelea banda la mamlaka hiyo katika maonyesho ya 38
ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Kumbukumbu ya Mwalimu
Nyerere maarufu Sabasaba vilivyopo katika barabara ya Kilwa.
“Tunahitaji watanzania wajivunie mafanikio haya na kuchangamkia
fursa za uwekezaji zinazoendelea kukua siku hadi siku,” alisema.
Alisema viwanda vilivyowekeza katika maeneo hayo vinazalisha
bidhaa zenye viwango vya kimataifa na kuuzwa katika masoko ya kimataifa na
kuiongezea nchi fedha za kigeni na ajira kwa watanzania.
Alisema hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kubwa kwa vile kwa muda
mrefu Tanzania ilikuwa hainufaiki na mazao yake kwa vile yaliuzwa bila ya kuyaongezea
thamani.
Mwanzo tulikuwa nyuma katika utumiaji wa fursa za maeneo haya,
sasa wawekezaji wamekuwa mstari wa mbele katika kuyatumia,”alisema.
Pia alisema mikoa ambayo ilikuwa inasuasua kutoa maeneo kwa ajili
ya maeneo maalumu kwa ajili ya mmalaka, sasa wakati umefika kufanya hivyo kwa
faida ya taifa.
Viwanda mbalimbali ambavyo vimewekeza chini ya leseni ya mamlaka
ya EPZA vinashiriki maonyesho hayo vikiwemo Mazava cha Morogoro, Tanzania Tooku
Garments Co. Ltd cha Dar es Salaam, Fresh Air Ltd, na Power Flour Ltd.
Akitembelea maonyesho hayo mwishoni mwa wiki, Rais Jakaya Kikwete
pia alipita katika banda la mamlaka hiyo.
Mwanzoni mwa wiki iliyopita, ilitangazwa mshindi na kupata makombe
katika maeneo mawili tofauti ya uendelezaji viwanda pamoja na kukuza biashara
katika kundi la bidhaa za mauzo ya nje.
Uongezaji thamani mazao ya kilimo ni moja ya eneo linaloongoza kwa
uwekezaji wa viwanda chini ya Mamlaka ya EPZA.
Kwa wastani, viwanda vilivyowekeza hadi sasa asilimia takribani 55
inahusisha uongezaji thamani mazao ya kilimo pamoja na ujenzi wa viwanda
vya useketaji wa nguo.
Maeneo mengine yanayovutia wawekezaji kuwekeza chini ya mamlaka
hiyo ni pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ngozi za wanyama ambazo hutumika
kutengenezea bidhaa mbalimbali.
Mwisho
No comments:
Post a Comment