Tuesday, July 15, 2014

Wakurugenzi wahimizwa kuzingatia mafunzo


Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakurugenzi ya Tanzania, Bw. Said kambi akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.  Taasisi hiyo inaendesha mafunzo ya siku tano yanayolenga kuwajengea uwezo wakurugenzi na viongozi wengine wakiwemo wajumbe wa bodi mbalimbali toka sekta za umma na binafsi.
Muwezeshaji wa Taasisi ya Wakurugenzi ya Tanzania, Dr. Kasim Husein (kushoto) akielezea jambo wakati wa mafunzo yanayoendeshwa na taasisi hiyo jana Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.  Taasisi hiyo inaendesha mafunzo ya siku tano yanayolenga kuwajengea uwezo wakurugenzi na viongozi wengine wakiwemo wajumbe wa bodi mbalimbali toka sekta za umma na binafsi.

Na Mwandishi wetu, Pwani

Viongozi mbalimbali wa mashirika na kampuni katika sekta za umma na binafsi wametakiwa kuhakikisha kuwa wanazingatia mafunzo ya mara kwa mara ili kumudu majukumu yao vyema kwa faida ya taasisi zao na nchi kwa ujumla.


Imesemekana kuwa uhitaji huo ni muhimu sana kwa sasa hasa ambapo dunia inabadilika kwa haraka na umuhimu wa kubadilishana taarifa ni mkubwa kwa ufanisi wa viongozi hao.


Akiongea na waandishi wa habari jana mjini Bagamoyo, Mkoani Pwani, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Wakurugenzi ya Tanzania, Bw. Said kambi alisema kuwa siku za kufikiria kuwa viongozi wanazaliwa zimekwisha.

“Kiongozi anaandaliwa na kutayarishwa,” alisema.

Taasisi hiyo inaendesha mafunzo ya siku tano yanayolenga kuwajengea uwezo wakurugenzi na viongozi wengine 14 kama vile wajumbe wa bodi mbalimbali toka sekta za umma na binafsi.

Mafunzo hayo yako chini ya Programu ya taasisi hiyo inayojulikana kama Stashahada ya Wakurugenzi ambapo baada ya kufuzu washiriki hupatiwa vyeti na kuwa wanachama wa taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Bw. Kambi hadi sasa jumla ya wakurugenzi 300 wameshafaidika na mafunzo hayo yanayowahikikishia kupata utaalamu bora zaidi wa menejimenti.

Kwa mujibu wa afisa huyo, kozi hiyo inawawezesha washiriki kupata msingi wa utawala bora wa mashirika; mbinu za kuweza kukabiliana na majukumu yao; kufahamu sheria na taratibu zinazohusu uendeshaji wa mashirika na kampuni; kufahamu zaid kuhusiana na kuandaa mipango kabambe; na kufahamu kuhusu taarifa za fedha miongoni mwa mambo mengine muhimu.

Alisema kuwa mafunzo hayo yanazingatia sana kujifunza kwa kushughulikia mifano halisi, majadiliano na miradi halisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Bw. Pius Maneno alisema kuwa tathmini ya mafunzo yanayotolewa na chombo hicho tangu kizinduliwe mwaka 2012 ni nzuri.

Bw. Maneno alisema taasisi hiyo inayowalenga wakurugenzi na maafisa waandamizi inataka kuimarisha uendeshaji wa mashirika Tanzania.

No comments: