Thursday, July 3, 2014

Maghembe ahaidi miundombinu ya maji Kilimanjaro, Tanga

Waziri wa Maji ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe akisalimiana na watendaji wa ngazi mbalimbali katika kata ya Kriya, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjarao wakati alipotembelea na  kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali hivi karibuni.
Waziri wa Maji ambae pia ni mbunge wa Jimbo la Mwanga Profesa Jumanne Maghembe (kulia), akifurahia jambo na Mzee Juma shabani Hamisi Mkzi wa kijiji cha Tologha katika kata hiyo wakati alipotembelea na  kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya nne katika kata zilizopo katika Jimbo la Mwanga hivi karibuni.
Na Mwandishi Wetu , Mwanga
Serikali inatarajia kutumia jumla ya shilingi bilioni 140 kwa ajili ya kuvipatia  maji safi na salama vjiji 38 vilivyopo katika wilaya za Mwanga, Same na Korogwe katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Utakapokamilika, mradi huo unatarajiwa kuleta nafuu kubwa katika vijiji hivyo ambavyo vimekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu.

Akizungumza na wananchi wa kata za Kigonigoni, Tologha na Lembeni wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro hivi karibuni, Waziri wa Maji ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe, alisema mradi huo mkubwa wa maji ni moja ya utekelezaji wa mkakati wa serikali  wa Matokeo Makubwa Sasa.

“Serikali inatekeleza mradi huu mkubwa wa maji kutoka Nyumba ya Mungu na kupeleka katika vijiji hivyo ambavyo vina matatizo makubwa ya maji,” alisema Profesa Maghembe.

Aliongeza kua mradi huo utakapokamilika utakua umetatua tatazo la maji Kwa vijiji 28 vya wilaya ya Mwanga na vijiji vingine 10 kutoka katika wilaya za korogwe na Same.

“Hivi sasa tatizo la maji ni kubwa sana katika maeneo mengi katika wilaya ya Mwanga, naamini miradi hii yote itakapokamilika Mwanga itakua haina tena shida ya maji kama ilivyo sasa,” aliongeza.

Alisema tayari kwa sasa kuna kampuni za kandarasi 23 zilizoomba kufanya kazi hiyo na kuwa kinachofanyika sasa ni kazi ya kuwachuja ili kuwapata 3 wenye sifa za kufanya kazi hiyo.

“Hivi sasa tunafanya kazi ya kuwachuja ili wabaki 3 kati ya wale walioomba na ifikapo mwezi Septemba mwaka huu kazi itaanza rasmi” alisema Profesa.
“Ndugu zangu naomba muwe wavumilivu kidogo, jambo hili sio la mara moja linahitaji muda na mambo yatakapokamilika maji yatakua ya uhakika katika wilaya yetu,”alisema.

Aidha Waziri huyo alizitaja kata za Tologha, Msangeni,Raa, Butu, Kisangara, Shigatini, Usangi na Kifura kuwa kuna miradi inatekelezwa kwa sasa na kazi ya ujenzi inaendelea katika baadhi ya maeneo ya kata hizo zilizopo Wilaya ya Mwanga.

“Miradi hiyo yote ambayo nimeorodhesha itagharimu jumla ya shilingi bilioni 350 za kitanzania, hivyo ni vema wananchi mkajua kuwa serikali inafanya kazi kwa maslahi yenu,” alisema.

Wakizungumzia miradi hiyo inayotekelezwa na serikali katika Wilaya ya  Mwanga, baadhi ya wananchi walisema jambo hilo ni zuri na kuwa serikali inahitaji kupewa ushirikiano na wananchi wa maeneo husika ili kuweza kulinda rasilimali hiyo muhimu.

“Mimi kwangu naona ni jambo kubwa sana, namshukuru waziri kwa jitihada zake,” alisema Ramadhani Juma mkazi wa kata ya kigonigoni.

Alisema kinachotakiwa ni viongozi wa kata hizo kutoa ushirikiano kwa wasimamizi wa miradi ili wasifanye kazi katika mazingira magumu kwani wananchi ndio wanatakiwa kuwa wa kwanza kutoa ripoti pale inapotokea hujuma.


Mwisho  

No comments: