Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu juu na mingine
inayoendelea inatarajiwa kuleta ahueni kubwa ya huduma za maji katika jiji la
Dar es Salaam mara itakapokamilika.
Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam
kuhusiana na miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali, katika ziara ya
Naibu waziri wa Maji Mhe. Amos Makalla hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi wa
Ufundi wa DAWASA Mhandisi Romanus
Mwang’ingo alisema mradi wa upanuzi wa
mtambo wa Ruvu juu ilianza rasmi tarehe 15 mwezi wa pili mwaka huu na itagharimu
shilingi bilioni 65.11.
“Matarajio ni kumaliza kazi mwezi August 2015…upanuzi wa
mtambo ukikamilika utaongeza uzalishaji kutoka lita milioni 82 hadi lita
milioni 196,” alisema, na kuitaja kampuni inayojenga mradi huo kama VA TECH
WABAG ya India.
Akielezea zaidi alisema mkandarasi ameanza kazi mbalimbali za
matayarisho pamoja na kazi ya ujenzi wa eneo jipya la kuchujia maji
lijulikanalo kitaalamu kama ‘Clarifier’.
Akielezea ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji Kutoka Ruvu
juu Kwenda Kibamba na hatimaye Kimara, Mhandisi huyo alisema tayari mkataba
kati ya DAWASA na kampuni ya Megha Engineering and Infrastructural Ltd kutoka
India ulishasainiwa tangu mwezi wa kwanza mwaka huu na kuwa mradi huo
unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 18.
Alisema mradi huo utakaogharimu shilingi 97.3 bilioni ulianza
rasmi mwezi wa tatu mwaka huu na matarajio ni kumaliza kazi mwezi Septemba
2015.
Alifafanua kuwa kazi zitakozohusika katika mradi huu ni
pamoja na ujenzi wa bomba jipya kutoka Ruvu juu hadi Kibamba lenye kipenyo cha
milimita 1200 (mita 1.2) na urefu wa kilomita 20 na bomba jipya kutoka Kibaha
Tanita hadi Kibamba hadi Kimara lenye
kipenyo cha 1000mm na urefu wa kilomita 10.
Pia itahusisha ujenzi wa tenki jipya Kibamba lenye uwezo wa
kuhifadhi maji lita milioni 10, na ukarabati au ujenzi wa matenki mawili ya
Kimara.
“Mkandarasi amekamilisha upimaji na ameanza kutengeneza
mabomba huko India na ameanza ujenzi wa jengo la ofisi ya mradi Kibaha,”
alisema.
Akizungumzia upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji na
Kuunganisha Wateja, Mwang’ingo alisema upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji
katika maeneo yaliyo kandokando ya mabomba makuu kutoka Ruvu Chini na Ruvu Juu
utaanza Septemba 2014.
“Maeneo yatakayonufaika na awamu hii ni vitongoji vilivyopo
kati ya mji wa Bagamoyo hadi eneo la Tegeta na vitongoji vilivyopo kati ya mji
wa Mlandizi na maeneo ya Mbezi na Kimara,” alisema na kuongeza kuwa kazi hii
itatekelezwa kwa fedha kutoka India.
Makisio ya kihandisi yanaonyesha kuwa gharama itakuwa ni
shilingi bilioni 40.
Alisema awamu itakayofuata ni upanuzi wa mfumo wa usambazaji
maji katika maeneo yote ya jiji yatakayopata maji kutoka Kimbiji na Mpera,
pamoja na maeneo ya jiji yasiyo na mabomba ya usambazaji.
“Mchakato wa kupata mshauri atakayesanifu na kutayarisha
vitabu vya zabuni za ujenzi unaendelea,” alisema.
Alisisitiza kuwa matarajio ni kukamilisha usanifu Desemba
2014 na kuanza kazi ya ujenzi wa mtandao wa majisafi kuanza Januari 2015 na kukamilisha hatua kwa hatua kuanzia
Desemba 2015 hadi Juni 2016.
Mwisho
No comments:
Post a Comment