Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Taasisi za
Wakurugenzi Afrika ( ACGN) ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya
Wakurugenzi Tanzania (IoDT), Bw. Said Kambi akisisitiza Jambo kwa waandishi wa
habari juu ya Tanzania kuwa Mwenyeji wa mkutano mkubwa wa bara la
Afrika,utakaofanyika jijini Dar es Salaam wiki Ijayo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa
mkutano mkubwa wa Mtandao wa Taasisi za Wakurugenzi Afrika (ACGN) kwa siku tatu
kuanzia tarehe 23 mwezi huu jijini Dar es Salaam.
Akitangaza mkutano huo jana jijini
Dar es Salaam, Afisa Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wakurugenzi ya Tanzania (IoDT),
Bw. Said kambi alisema mkutano huo utakutanisha viongozi wa mtandao huo.
Taasisi ya Wakurugenzi ya Tanzania ambayo ni
moja ya waanzilishi wa mtandao huo ndio watakuwa wenyeji wa mkutano huo.
ACGN iliundwa kujenga uwezo wa
wanachama wake kuimarisha uendeshaji wa mashirika, na kujenga mashirika bora
barani Afrika miongoni mwa mambo mengine.
Mtandao huo pia unatoa fursa kwa watunga
sera na wadau wengine kujadiliana kuhusiana na maswala mbalimbali yanayohusiana
changamoto mbalimbali zinazohusiana na uendeshaji wa mashirika na kampuni
barani Afrika.
Kwa mujibu wa Bw. Kambi ambaye pia
ni Makamu Mwenyekiti wa mtandao huo, mkutano utatanguliwa na futari kwa
washiriki na maafisa waandamizi wa makampuni walioalikwa hapa nchini siku ya
tarehe 23 kabla ya kuanza kwa mkutano rasmi siku inayofuata.
“Tunatarajia kutambulisha wajumbe na
washirika wapya wakati wa mkutano huo,” alisema.
Alitaja wajumbe wapya wanaotarajiwa
kutambulishwa kama Taasisi za Wakurugenzi toka nchi za Misri, Ethiopia, Tunisia
na Algeria.
Aliwataja washirika wapya kama Ethics Institute of South Africa (EISA), Association
of Chartered Certified Accountants (ACCA), na African Security Exchanges
Association (ASEA).
Pia alisema katika mkutano huo, ACGN
itatiliana saini makubaliano ya ushirikiano na taasisi mbalimbali zikiwemo International
Finance Corporation (IFC), EISA, ACCA, ASEA na Ernst &Young (EY).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa IoDT, Bw. Pius Maneno alisema uendeshaji
bora wa mashirika barani Afrika ni muhimu sana kwa sasa ambapo biashara
miongoni mwa mataifa ya Afrika inakuwa na pia mitaji ya uwekezaji barani humo
inazidi kuongezeka.
“Imeonekena
kuna umuhimu wa kuwa na mikakati ya kutengeneza miongozo ya uendeshaji
mashirika ili kuchochea biashara na kuwa na viwango vya kimataifa barani
Afrika,” alisema.
ACGN
ilizinduliwa nchini Mauritius mwezi wa Kumi mwaka jana.
Waanzilishi
wa mtandao huo walikuwa ni Taasisi za Wakurugenzi toka nchi za Kenya, Malawi,
Mauritius, Morocco, Msumbiji, Afrika ya Kusini na Tanzania.
Wengine ni
taasisi toka Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Mtandao huu unalenga kujenga uwezo
wa taasisi wanachama na kuendeleza uendeshaji bora wa mashirika katika sekta
binafsi na umma barani Afrika.
Mwisho
No comments:
Post a Comment