Tuesday, July 8, 2014

Watanzania watakiwa kujenga utamaduni kuweka akiba benki

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imewataka wananchi kujenga utamaduni  endelevu wa kuweka akiba ya pesa wanazozipata kutokana na juhudi mbalimbali katika benki na taasisi za fedha zilizosajiliwa na Benki Kuu kwani ni njia salama na faida zake kwa maendeleo ya kiuchumi kwao na kwa nchi ni kubwa.

Wakiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, maafisa wa taasisi hiyo inayoendesha shughuli zake chini ya Benki Kuu ya Tanzania walisema utamaduni wa kuweka pesa benki pamoja na faida nyingine unajenga mahusiano ya kibiashara kati ya mteja na benki hivyo kujitengenezea mazingira mazuri ya kuweza  kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao mbalimbali za kiuchumi.

Meneja wa Fedha na Utawala wa taasisi hiyo, Bw. Richard Malisa alisema pia amana zinazowekwa na wateja katika benki na taasisi za fedha zinatoa fursa kwa vyombo hivyo vya fedha kuwa na uwezo mkubwa wa kukopesha makampuni na wafanyabiashara mitaji ya kuendeshea shughuli zao, na hivyo kuchochea kasi ya maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Umuhimu wa benki katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi ni sawa na umuhimu wa injini kwenye gari kwani hufanya kazi kubwa ya kuyaunganisha pamoja mahitaji ya wenye kutaka kupata mahali salama pa kutunza fedha yao kwa faida na wale wenye mahitaji ya kupata mitaji kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.  Tunatoa wito kwa wananchi kujenga na kuwa na utamaduni endelevu wa kuweka pesa zao benki kwani faida zake kiuchumi kwao binafsi na kwa nchi ni kubwa,” alisema.

Aliwatoa wasiwasi wananchi kuhusiana na usalama wa fedha zao akisema kuwa madhumuni ya taasisi hiyo ni kuhakikisha kuwa inalinda kwa mujibu wa sheria amana zao katika vyombo vya fedha vilivyopewa leseni ya biashara na Benki Kuu na inawajibika kuwalipa fedha zao zote au sehemu yake kama ilivyoainishwa na sheria pale ambapo moja ya benki imefilisika na kushindwa kuendela na shughuli zake.

Akiendela kuelezea majukumu ya taasisi hiyo, Meneja wa Uendeshaji wa chombo hicho, Bi. Rosemary Tenga alisema taasisi hiyo ina jukumu la kukusanya michango kutoka kwa wanachama wake ambao ni benki na taasisi zote za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu kwa madhumuni ya kendelea kuutunisha Mfuko wa Bima ya Amana.

Pia alisema taasisi hiyo ina wajibu wa kuwekeza kwenye dhamana za serikali fedha zinazokusanywa kama michango kutoka kwa wanachama na faida inayopatikana kwenye uwekezaji huu huwa ni chanzo kimojawapo cha mapato ya taasisi hii.

“Pia tunasimamia ufilisi wa benki au taasisi ya fedha iliyofilisika pale ambapo taasisi hii imeteuliwa na Benki Kuu kufanya  kazi hiyo,” alieleza.

Bi. Tenga aliwataka wanafunzi kuanza kujenga utamaduni endelevu wa kujiwekea akiba vyombo vya fedha vilivyo sajiliwa na Benki Kuu kwa usalama na maendeleo yao na ya nchi kwa ujumla.

“Huwezi kujua litakalotokea mbele, ni muhimu kujenga mazoea ya kujiwekea akiba kwa kila kipato kwa kuwa si tu itasadia kutatua matatizo yaliyo mbeleni ambayo hujayajua kwa sasa, bali pia kama mkakati makini na endelevu wa kujijengea uwezo binafsi wa kujipatia raslimali kwa maisha yaliyoko mbele,” alisema afisa huyo.

Bodi ya Bima ya Amana ilianza kazi mwaka 1994.

Mwisho

No comments: