Wednesday, July 2, 2014

Watanzania washauriwa kudumisha umoja, mshikamano

Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emmanuel Ole Naiko (wa pili kushoto) akiwa na Paroko wa Parokia ya Mt. Peter, Padri Stephen Kaombe (kulia) wakati wa kuchangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha huduma cha Kadinali Laurean Rugambwa cha parokia hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Wengine ni Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Dk. Adelhelm Meru (kushoto) na Bw. David Molel (wa pili kulia). Jumla ya Tshs milioni 52 zilipatikana.
Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emmanuel Ole Naiko (wa pili kulia) akiwa na Mwenyekiti wa Parokia ya Mt. Peter, Dk. Adelhelm Meru (kushoto) wakati wa kuchangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha huduma cha Kadinali Laurean Rugambwa cha parokia hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Wengine ni Bw. David Molel (kulia) na Bi. Ruth Molel (wa pili kushoto). Jumla ya Tshs milioni 52 zilipatikana.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Watanzania wameshauriwa kuzidi kuendeleza upendo miongoni mwao bila ya kubaguana kwa misingi ya rangi, kabila na dini ili kuendeleza jamii na nchi kwa ujumla.

Akiongea wakati wa kuchangisha pesa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha huduma cha Kadinali Laurean Rugambwa cha parokia ya Mt. Peter jijini Dar es Salaam, Balozi wa Heshima wa Botswana nchini Tanzania, Bw. Emmanuel Ole Naiko alisema upendo na mshikamano miongoni mwa wananchi ndiyo msingi mkuu wa maendeleo.

“Tukizidi kuendeleza upendo miongoni mwetu tunakuwa na fursa ya kutoulizana tofauti zetu za kabila, rangi na dini na badala yake tutaendelea kuishi kwa misingi ya utanzania,”alisema.

Alisema hakuna sababu ya watanzania kuulizana na kubaguana kwa misingi hiyo badala yake waishi kama wamoja na kumtukuza Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliyeumba wanadamu.

Aliwataka wakrito na watu wote kuchangia shughuli za kidini ili kuweza kufanikisha shughuli mbalimbali za kijami, kichungaji na kiuchumi.

Balozi huyo katika sherehe hiyo aliweza kuchangisha kiasi cha Tshs milioni 52 kati ya lengo la Tshs 330 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo hicho.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Dkt. Adelhelm Meru ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) alisema kituo hicho kitatagharimu kiasi cha Tshs bilioni 2.6 kitakapokamilika.

Alisema kituo hicho kimepewa jina la Kadinali wa kwanza wa Afrika na Tanzania, Laurean Rugambwa kama kumbukumbu na heshima kwake.

Alisema kituo hicho kilianza kujengwa miaka 10 iliyopita kwa waumini kuchangishana na inatarajiwa kuwa hatimaye mwaka huu kitakamilika.

Naye Paroko wa Parokia hiyo, Padri Stephen Kaombe alisema waumini wake walifanya sherehe ya somo wa parokia, Mt. Petro ili kuchangia mavuno kwa ajili ya kupata fedha kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.

“Leo wakristo na watu wote wameshiriki kuchangia ujenzi na tunatarajia hivi karibuni ujenzi utakamilika,”alisema.
Alisema Parokia kupitia Mt. Petro itazidi kuwaombea waumini wake na watu wote ili amani na baraka katika mwaka huu wa familia vipatikane.


Mwisho

No comments: