Wednesday, July 2, 2014

Matokeo Makubwa Sasa ni muhimili utekelezaji miradi ya PPP-Nagu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dkt. Mary Nagu, ameuelezea Mpango wa Matokea Makubwa Sasa ‘ Big Results Now’ (BRN) kama chachu katika ufanikishaji wa utekelezaji wa Miradi ya Ubia kati ya Sekta za Umma na Binafsi (PPP).

Waziri Nagu alisema hivi karibuni jijini Dar es Salaam kuwa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa itakuwa ni kipimo na kichocheo katika utekelezaji wa miradi yote inatekelezwa kwa ubia wa wa sekta hizi kubwa za umma na binafsi.

“Serikali ilishakamilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya PPP ya mwaka 2010 ilikuunganisha Vitengo vya PPP na kuwa na Kitengo kimoja chenye uwezo na mamlaka ya kuidhinisha utekelezaji wa miradi ya PPP,” alisema.

Dkt. Nagu amesema kuwa serikali imeshapendekeza uanzishwaji wa Mfuko wa Kuwezesha Utekelezaji wa miradi ya PPP utakaojulikana kama ‘PPP Facilitation Fund’ ambao kimsingi utasaidia Mamlaka za serikali kuandaa upembuzi yakinifu utakaozingatia vigezo vya uwekezaji kwa utaratibu wa PPP.

“Ni ukweli usiopingika kuwa nchi nyingi duniani ikiwepo India zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kutumia mfumo au utaratibu huu kutokana na vipaumbele vyake vya maendeleo,” alisema na kuongeza kuwa utaratibu huu unajulikana kama   ‘viability gap funding’ na kazi yake kubwa ni kuzijengea uwezo sekta za umma na binafsi.

Dkt. Nagu aliongeza kuwa mfuko huu ‘ viability gap funding’ utasaidia sana kuzijengea uwezo mamlaka za sekta za umma na binafsi pamoja na kuwepo changamoto katika utekelezaji miradi ya PPP.

Kwa mujibu wa Waziri Nagu, Serikali ya Awamu ya Nne chini Rais Dkt. Jakaya Kikwete imedhamiria kutekeleza miradi mingi mikubwa kwa ubia kati ya sekta za umma na binafsi ilikufikia malengo ya maendeleo kwa faida ya taifa na watu wake wote.

Miradi ambayo utelekelezaji wake utakuwa chini ya Matokeo Makubwa Sasa ni Mradi wa Umeme Kinyerezi 3 na Kinyerezi ,Mradi wa Umeme wa Masigira , Mradi wa Umeme wa Rumakali , Mradi wa Umeme wa Rusumo , Mradi wa Umeme wa Ruhuji  pamoja Mradi mkubwa wa  Stiegler’s Gorge.

Mingine ni ukarabati mkubwa wa Gati namba moja mpaka saba pamoja na ujenzi wa Gati mpyanamba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Kuboresha  Bandari ya Mtwara, ujenzi wa Kituo cha Shehena Kisarawe (Container Freight Station) ,  Ujenzi wa Bandari Mpya Bagamoyo na kuendeleza Eneo la Ukanda Maalumu wa Uwekezaji Bagamoyo (Export Processing Zone (EPZ) ambayo yote hii utekelezaji wake utakuwa chini ya Matokeo Makubwa Sasa ilikufikia malengo yaliyokusudiwa.

Dkt. Nagu ametaja miradi mingine mikubwa kuwa ni Ujenzi wa Reli ya Mchuchuma-Liganga , Uboreshaji wa Reli ya Tanga-Arusha, Ujenzi wa Reli Mpya ya Arusha-Musoma ,Ujenzi wa Barabara ya Chalinze-Dar es Salaam , Ujenzi wa Jengo jipya  la Tatu la Abiria kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Upanuzi wa Viwanja vya Ndege vya Arusha , Mwanza, Mtwara ,Songwe na Kilimanjaro  ilikudhi viwango vya kimataifa na kupokea ndege nyingi zaidi kwa wakati mmoja.

Ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa reli za Dar es Salaam-Isaka-Keza-Musongati,Tabora-Kigoma,Uvinza-Musongati,Mpanda-Karema,Isaka Mwanza. Pia mradi wa kuunganisha Bandari mpya ya Mbegani kwa reli pamoja na kuunganisha relin ya TAZARA na Bandari za Kasanga,Kigoma na Mwanza.

Matokeo Makubwa Sasa inalenga kuleta mbinu mpya za utendaji kazi wenye lengo haswa la kuweka muda maalum wa utekelezaji wa jambo au mradi ambao umepitishwa bila ya kucjelewa.

Zipo Sekta sita za uchumi ambazo zimelengwa chini ya usimamizi wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na sekta hizo ni za elimu, nishati, kilimo, usafirishaji, maji na kukusanya raslimali yaaani ‘resource mobilization’.

Kuundwa kwa kwa kifungu cha Sheria ya PPP ni matokeo ya kuwepo kwa Sera ya ubia kati ya sekta za umma na binafsi ambayo iliundwa mwaka 2009.

Mwaka mmoja baadaye Kifungu cha Sheria Namba   18 kikaundwa na kuanzishwa kwa vitengo vya PPP chini ya uratibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha.

Mpango wa Ubia kati ya sekta ya Umma na ile sekta Binafsi unalenga kukabiliana na changamoto zilizopo mbele katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na ile Dira ya Maendeleo ya 2025.

Mwisho.


No comments: