Wednesday, July 2, 2014

Wafanyabiashara, wawekezaji toka China watakiwa kudumisha mahusiano

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wafanyabiashara na wawekezaji wa China hapa Tanzania wametakiwa kufanya kazi zao katika misingi ambayo itadumisha na kuimarisha mahusiano mema ya kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili.

Makamu wa Rais wa China, Bw. Li Yuanchao alitoa ujumbe huo alipokuwa akitembelea kiwanda cha nguo cha Tanzania Tooku Garments Co. Ltd kinachomilikiwa na raia wa China jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Kiongozi huyo alitembelea kiwanda hicho alipokuwa katika ziara kwenye Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji (EPZA).

Kiwanda hicho cha nguo ni moja ya vilivyowekeza katika eneo hilo la EPZA.
Bw. Yuanchao alisema kuwa Tanzania na China zina uhusiano wa kihistoria ambao hauna budi kuimarishwa sasa.

“Tunataka viwanda kutoka nchini kwetu viwe ni sehemu ya kukuza ajira, ujuzi na kuleta teknolojia hapa,”alisema.

Alisema kiwanda hicho kikiendelea vizuri pia kitavutia wafanya biashara wa nchi yake kuja kuwekeza Tanzania na kwa kufanya hivyo nchi zote mbili zitafaidika.

“Nimekuja katika kiwanda hiki kuona uzalishaji na nimeona kinaendelea vyema na hii inanipa imani kuwa wawekezaji toka China wanafanya vizuri,”alisema.

Akiwa katika maeneo hayo ya EPZA pia aliongea na wafanyakazi na uongozi wa kiwanda na viongozi wa serikali.

Waziri wa Biashara na Viwanda, Dkt. Abdallah Kigoda alisema mchango wa kiwanda hicho kwa uchumi ni mkubwa.

“Kiwanda hiki kimeajiri watu 1000 na kuna mpango wa kupanuliwa zaidi ili kiweze kuajiri kati ya watu 2,000 hadi 3, 000,”alisema.

Kiwanda hicho kinazalisha nguo mbalimbali na kinauza katika soko la Marekani.

Alisema jambo zuri ni kuwa kiwanda hicho wafanyakazi wake wengi walioajiriwa ni wanawake ambao wanahitaji sana kupatiwa kipaumbele katika ajira.

Alisema matarajio ni kwamba kiongozi huyo ataenda kuwa balozi mzuri nchini kwake na kuvutia zaidi wawekezaji wengine nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru alisema wawekezaji kutoka nchini China wanakaribishwa kuwekeza katika maeneo ya mamlaka hiyo ambayo yameshatengwa kwa ajili hiyo katika mikoa mbalimbali.

“Tunawakaribisha muwekeze katika maeneo huru ya uwekezaji Tanzania,” alisema.

Alisema katika kipindi cha miaka sita iliyopita mamlaka yake imezalisha ajira 32,000, viwanda vilivyowekeza 118 na hadi sasa tayari mtaji umefikia zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 1.3.

Alisema mamlaka inaendelea kuvutia wawekezaji katika maeneo yake ikitilia mkazo hasa maendeleo ya viwanda.

Akiwa hapa nchini katika ziara yake ya siku sita, kiongozi huyo alifungua kongamano la biashara kati ya nchi hizo mbili na kushirikisha kampuni zaidi ya 100 kutoka China na kampuni zaidi ya 120 za kitanzania.

Mwisho



No comments: