Wednesday, July 2, 2014

Wananchi Mwanga watakiwa kulinda amani

Na Mwandishi Wetu, Mwanga

Wananchi katika wilaya ya Mwanga wametakiwa kuhakikisha wanailinda amani iliyopo kwani ni moja ya msingi mkubwa wa maendeleo.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe ambaye alikuwa katika wilaya hiyo kukagua miradi ya maendeleo.

Prof. Maghembe ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mwanga alisema mwishoni mwa wiki kuwa kuwepo kwa maendeleo ya kweli na mshikamano katika kujenga taifa la Tanzania na watu wake kunategemea amani.

“Ndugu zangu ni amani ambayo itatufanya tuendelee kupiga hatua za maendeleo ya nchi hii, tuilinde,” alisema.

Akiongelea maendeleo katika wilaya hiyo, Prof. Maghembe alisema katika kipindi cha mwaka 2000, watoto 320 walienda kidato cha kwanza na kuwa idadi hiyo imeongezeka mara dufu.

Alisema kutokana na idadi ya watoto wanaoingia kidato cha kwanza kuongezeka, sasa vijana zaidi ya 1000 wanakwenda kitado cha sita katika wilaya hiyo.

“Sekta ya elimu imeendelea kukua katika wilaya hii, leo hii ukiulizia watoto walioko katika vyuo vikuu kutoka katika wilaya hii sio wa kubabaisha idadi yao ni kubwa,”aliongeza.

Mbali na Prof. Maghembe kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika jimbo hilo la Mwanga pia alitumia wasaa huo kuimarisha uhai wa chama cha mapinduzi katika maeneo mabalimbali ya jimbo hilo.

Baadhi ya wananchi wa jimbo la mwanga walielezea mafanikio mbali mbali yaliyopatikana katika kipindi cha awamu ya nne katika sekta ya elimu na kusema makubwa yamefanyika hivyo  ni vema wananchi wakaunga mkono juhudi hizo.

“Kwa kweli ni jambo la kujivunia kwa sasa watoto wetu wengi sasa hivi wanakwenda kidato cha sita hadi vyuo vikuu,”alisema Hamisi Mndeme mkazi wa kijiji cha Mangio kata ya Mwaniko.

Allisema shule za kata zilizojengwa zimekuwa mkombozi mkubwa kwa sasa japo hapo awali kulikua na matatizo ya walimu na kuongeza kuwa kwa sasa shida ya walimu sio kubwa.

“Mwanzoni tulikua na tatizo la walimu kwa sasa sio tatizo kubwa, shida yetu kubwa ni walimu wa sayansi,”alisema Mndeme.

Naye Bi. Sara Msuya ambaye ni mkazi wa kata ya Kifura alisema wanashukuru kwa serikali kuwapelekea zahanati jambo ambalo litapunguza tatizo la wakina mama kujifungulia majumbani na kusaidia kupunguza vifo vya mara kwa mara vya mama na mtoto.

“Tulikua na matatizo makubwa ya kujifungulia nyumbani, kwa sasa tunashukuru hospitali ipo na tuna daktari wa uhakika katika zahanati yetu ya Kifura,” alisema Bi Sara.

Pia aliwataka watendaji katika ngazi mbalimbali katika kata za Chomvu, kighare na Kirongwe tarafa ya Usangi kuwaeleza wananchi shughuli mbalimbali za maendeleo zilizotekelezwa na serikali.

“Maendeleo ni hatua, ni lazima watu wakubali hilo, huwezi kubeza jambo ambalo hujaliona,” alisema Prof. Maghembe.

Aliwataka watendaji kutoona aibu kueleza yale yaliyofanyika, katika kipindi hiki hatua kwa hatua na kama jambo halijafanyika ni lini litatekelezwa ili kuepusha maswali mengi kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa ni haki ya mwananchi kujua serikali yao imefanya nini, hivyo ni jukumu la viongozi wa vijiji, vitongoji na kata kuyaeleza hayo kwani serikali imefanya mengi makubwa katika sekta za afya, maji na miundombinu ya barabara.

“ Watendaji wote mna wajibu wa kuwaeleza wananchi serikali iliyoyafanya katika kipindi hiki cha awamu ya nne,” alisisitiza.

Mwisho.




No comments: