Thursday, August 21, 2014

Sekta binafsi yaonyesha nia kushiriki vita dhidi ya ujangili

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Sekta binafsi nchini imesema ina nia ya kushiriki katika vita dhidi ya majangili wanaotishia maisha ya wanyama kama tembo na wengineo kupitia mfumo wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma (PPP).

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Bw. Godfrey Simbeye amesema jana jijini Dar es Salaam kuwa ujangili unatishia kuangamiza makampuni mengi binafsi katika sekta ya utalii.

Mwaka jana, TPSF ilikutana na waziri mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii na kuongelea maeneo mbalimbali ambayo sekta binafsi inaweza kutoa mchango kuboresha sekta hiyo.

“Tulidhani sisi kama sekta binafsi tuna mchango katika hili,” alisema Bw. Simbeye mara baada ya mkutano ngazi ya kitaaluma ambapo wadau mbalimbali walifahamishwa jinsi teknolojia inavyoweza kutumika kupambana na ujangili.

Katika kutekeleza nia yao, sasa TPSF kwa kushirikiana na kampuni ya Bathawk Recon ya hapa nchini iko katika mchakato wa kutoa mapendekezo kwa serikali kutumia teknolojia ya kisasa kabisa kupambana na ujangili hapa nchini.

Kwa kutumia teknolojia hiyo inayojulikana kama UAV Anti Poaching OPS, vyombo vidogo visivyo na rubani vitaweza kurushwa katika maeneo ya mbuga na hifadhi na kutoa taarifa kwa haraka iwapo kuna dalili za majangili na eneo gani na hivyo kurahisisha ufuatiliaji wao.

Alisema dhamira ya kutaka kuingia katika vita dhidi ya ujangili inatokana na kwamba kampuni nyingi zinafanya utalii na kutegemea kazi hiyo na kwamba kama wanyama watauawa wote basi hakutakuwa na utalii na kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta binafsi na nchi nzima kwa ujumla.

“Sekta ya utalii inachangia asilimia 17 ya pato la taifa na inatoa ajira kwa watu 300,000,” alisema.
Ni kutokana na mchango huo wa sekta ya utalii, sekta binafsi nchini kwa kushirikiana na kampuni hiyo iliyosajiliwa hapa nchini wameona ni vyema kuanza mchakato wa kuona uwezekano wa kufanya kazi na serikali kwa kutumia teknolojia hiyo kupambana na ujangili ambao sasa umekuwa janga la kimataifa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ya Bathawk Recon, Bw. Tom Lithgow, kampuni yake ina uwezo wa kuingiza teknolojia ya aina hiyo kufanya kazi kwa kushirikiana na serikali kutokomeza ujangili hapa nchini.

“Tukikubaliwa tutaleta vifaa hivi ambavyo vina uwezo wa kuzunguka angani vikifanya doria na kuleta taarifa mbalimbali sahihi zitakazofanyiwa kazi na mamlaka husika kwa haraka,” alisema.

Kwa sasa kampuni hiyo kwa kushirikiana na TPSF wako katika mchakato wa kuomba ruhusa ya kufanya majaribio ya teknolojia hiyo.

Kwa mujibu wa Bw. Lithgow, teknolojia hiyo inatumika nchini Afrika ya Kusini na inaendelea kuonyesha mafanikio wakati nchi ya Kenya iko katika hatua ya majaribio.

Alisema kudhibiti ujangili ndiyo njia pekee ya kuhakikisha wanyama kama tembo, faru na simba hawapotei katika uso wa dunia.

Mkurugenzi Msaidizi, Vita dhidi ya Ujangili, Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Wanyamapori, Bw. Julius Kibebe alisema kikao hicho cha ngazi ya kitaalamu kilikuwa cha mafanikio.

“Kama tulivyoelezwa na wataalamu hawa, teknolojia hii ina uwezo wa hali ya juu...tunahitaji suluhisho la aina hii,” alisema.

Alisema ushiriki wa sekta binafsi katika swala hili ni jambo la muhimu kwa vile unalenga kuongeza nguvu katika kutokomeza ujangili.

Alisema serikali inakaribia kukamilisha mkakati wa kitaifa wa kupambana na ujangili kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kwa kushirikiana na wizara mbalimbali na wadau wengine.

Pamoja na mambo mengine, akiwa ziarani nchini Uingereza mapema mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete aliomba msaada jumuiya ya kimataifa kupambana na ujangili kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Katika miaka ya karibuni swala ya ujangili limekuwa tete Tanzania na duniani kwa ujumla.

Mwisho   


No comments: