Tuesday, August 12, 2014

NEC yafafanua kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba, akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
  
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa ufafanuzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kuanza hivi karibuni linamhusu kila raia mwenye sifa ya kupiga kura.

Ufafanuzi huu unakuja wakati pakiwa na mawazo tofauti ya nani hasa anatakiwa kushiriki katika zoezi hilo huku baadhi ya watu wakidhani kuwa jambo hili linawahusu wale ambao hawakupata kujiandikisha kupiga kura au waliopoteza kadi au waliofikia umri wa kupiga kura.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva amesema jana jijini Dar es Salaam kuwa katika kufanya maboresho hayo na kupata daftari linaloaminika zaidi, Tume inatarajia kutumia mfumo mpya wa “Biometric Voters Registration System” au mfumo ambao utatumia utambuzi wa watu kwa alama za binadamu.

Kwa kutumia mfumo huu, muhusika atachukuliwa alama za vidole vyote vya mikono 10, picha na sahihi yake.

Hii ni tofauti na mfumo uliokuwa unatumika wa “Optical Mark Recognition” (OMR) ambapo muhusika alikuwa anajaza fomu na kuchukuliwa alama ya kidole kimoja tu ambao Jaji Lubuva anasema ulikuwa na uwezekano wa watu kujiandikisha hata mara mbili bila kutambulika.

“Watu wote wenye sifa watatakiwa kujiandikisha upya katika mfumo huu mpya na kupatiwa kadi mpya,” alisema.

Akitoa ufafanuzi zaidi alisema uboreshaji wa daftari hilo unatokana na matakwa ya kisheria na malalamiko ya wadau mbalimbali.

Alisema tangu kufanyika kwa uchuguzi mkuu mwaka 2010 pamekuwa na malalamiko toka kwa wadau mbalimbali kama vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wapiga kura wenyewe kuhusu haja ya kuboresha daftari hilo na kuondoa watu ambao hawastahili kuwamo kama waliofariki na kuongeza wengine wenye sifa.

“Malalamiko haya yanafanya imani ya watu juu ya daftari la wapiga kura iwe ndogo,” alisema.

Alifafanua kuwa sheria inaitaka NEC kuboresha daftari la wapiga kura mara mbili kati ya uchaguzi uliopita na uchaguzi unaokuja.

“Ni kutokana na matakwa ya kikatiba na sheria na malalamiko haya, NEC imelazimika kufanya zoezi hili kabla ya kura ya maoni na uchaguzi mkuu ujao 2015,” alisema.

Akizungumzia matayarisho ya zoezi hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Bw. Julius Mallaba alisema yanaridhisha na kuendelea vizuri.

Alisema maboresho ya daftari hilo kwa awamu hii ni mahsusi kwa ajili ya kura ya maoni kuhusu katiba mpya mapema mwaka 2015, uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 pamoja na chaguzi ndogo zitakazofuata baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Sehemu kubwa ya maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yamekamilika,” alisema.

Akielezea zaidi Bw. Mallaba alisema tayari NEC imeanzisha na kuhakiki vituo vipya na kuviweka katika ngazi ya vitongoji, vijiji na mitaa.

Vituo hivyo vimeongezeka kutoka vituo vya awali 24,919 na kufikia vituo 40,015 nchi nzima.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari ununuzi wa vifaa vya uandikishaji ikiwemo Biometric Voter Registration Kits umeshafanyika.

“Maandalizi ya melekezo kwa maafisa waandikishaji, waandishi wasaidizi pamoja na vyama vya siasa yameshafanyika,” alisema na kuongeza kuwa kanuni za uboreshaji zimeshaandaliwa.

Alisema kuwa maandalizi ya kituo cha kuhifadhia taarifa na mkakati wa utoaji wa elimu ya mpiga kura na machapisho mbalimbali tayari yameshakamilika.

Aliongeza kuwa katika maandalizi hayo, Tume imeshakutana na wadau mbalimbali kama wahariri, viongozi wa dini na vyama vya siasa ili kujadiliana na kupata maoni yao kuhusiana na zoezi hilo.

“Tunashukuru sana kwa michango ya mawazo yao…tunayapokea na kuyafanyia kazi,” alisema na kuongeza kuwa katika kuboresha zaidi, Tume inatarajia kukutana na makundi mengine kama vijana, kina mama na walemavu.

NEC imepewa jukumu la kisheria kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura na kuliboresha daftari hilo kwa ajili ya uchaguzi wa Rais na wabunge ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwisho


No comments: