Wednesday, September 24, 2014

Benki ya Afrika Tanzania yawataka wanafunzi kujenga tabia ya kusoma vitabu

Meneja Mwandamizi wa Benki ya Afrika Tanzania (BOA Bank), Tawi la Msimbazi (kariakoo), Bw. Emmanuel Mwaya akimkabidhi vitabu mbalimbali ambavyo vimetolewa na benki hiyo kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari  ya Penda Moyo Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Augenia Albano iliyopo Sokota wilayani Temeke jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Benki ya Afrika Tanzania imewataka wanafunzi nchini kujijengea tabia ya kusoma vitabu kama njia kuu itakayowawezesha kukuza upeo wao kiakili na kuweza kuchanganua mambo mbalimbali.

Meneja mwandamizi wa Benki hiyo, Tawi la Msimbazi, Bw. Emmanuel Mwaya alitoa ushauri huo alipokuwa akitoa msaada wa vitabu katika shule ya sekondari Penda Moyo iliyopo Sokota wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

“Lengo letu ni kutoa mchango wetu katika kukuza elimu,” alisema Mwaya mwishoni mwa wiki.

Alisema kuwa shule za umma zinachangamoto nyingi ambazo hushindwa kumudu gharama za elimu na kupelekea wanafunzi kukwama katika masomo yao.

“Tumeona tutoe mchango wetu kusaidia serikali katika kuendeleza sekta hii muhimu,” alisema.

Benki hiyo iko katika kampeni ya mwaka mzima ya kusaidia sekta ya elimu kwa kugawa vitabu katika shule mbalimbali nchi nzima.

“Elimu ndio msingi wa kila kitu...ni lazima mjitahidi kufanya vyema na kwa maendeleo yenu na taifa kwa ujumla,” alisema.

Aliongeza kuwa wingi wa vitabu mashuleni utasaidia kukuza viwango vya elimu na kupunguza changamoto za kielimu kwa ujumla.

Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Augenia Albano ameipongeza benki hiyo kwa kuwa na moyo wa kujikita katika kusaidia kukuza elimu ya nchi kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.

“Tutatumia vitabu kwa matumizi sahihi katika shule yetu,” alisema.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Yerusalem Bagaza ametoa shukrani zake kwa benki hiyo na kuwaomba wadau mbalimbali zaidi kujitokeza kwa wingi katika kusaidia sekta hiyo.

“Tunaahidi kuvitumia vitabu hivi vizuri ili vitumiwe pia na wenzetu watakaokuja baadae,” alisema.

Benki ya Africa Tanzania ilianzishwa miaka zaidi ya 30 Bamako, Mali.
Kwa hapa nchini ina zaidi ya miaka nane tangu ianzishwe ikihudumia makapuni makubwa pamoja na wafanyabiashara wa kati na wadogo.
Ina matawi nane jijini Dar es Salaam na mengine katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mtibwa, Mbeya, Tunduma, Mwanza, Kahama na Mtwara.


Mwisho

No comments: