Na mwandishi wetu, Dar es salaam
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) imesitisha udahiIi wa wanafunzi
wapya kwa mwaka wa masomo 2014/15 katika Chuo kikuu cha kimataifa cha Tiba na
Teknolojia (IMTU).
Uamuzi huo unatokana na chuo hicho kushindwa kutimiza
masharti mbalimbali, ikiwemo kutokuwa na wahadhiri wa kutosha na wenye sifa
stahiki kama inavyotakiwa na kanuni ya 15 ya sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka
2013.
Katika taarifa yao ya vyombo vya habari iliyosainiwa na Kaimu
Katibu Mtendeji wa tume hiyo ,Profesa Mugisha Mgasa imesema baada ya tume
kupokea taarifa ya timu iliyo tathmini ubora wa chuo hicho kati ya Agost 25
hadi 28, mwaka huu na wao kufanya ukaguzi,ilibainisha kuwa IMTU imekuwa na
mwendelezo wa matukio yasiyoridhisha.
Taarifa hiyo ilielezwa kuwa, TCU imekuwa ikitoa mwongozo kwa
chuo hicho kuhusu namna bora ya kutoa elimu ya juu, lakini kimekuwa kikikiuka
kutoa viwango bora vya elimu.
Upungufu unaoelezwa ni kudaili wanafunzi wengi zaidi ya
uwezo,upungufu wa vifaa pamoja na miundombinu ya kujifunza ,kuendesha kozi
ngazi ya cheti (UQF) level 6 bila ithibati na kukaidi agizo la tume la
kusitisha utoaji wa kozi hiyo.
IMTU pia inadaiwa kufanya taratibu za udahili wa wanafunzi
bila kufuata utaratibu wa TCU na uwapo wa wimbi la wahadhiri kuachishwa ama
kuanza kazi mara kwa mara,kitendo kinachofanya chuo hicho kuwa na uhaba wa
wahadhiri wenye sifa.
TCU pia imetoa notisi ya miezi mitatu kurekebisha upungufu
uliopo na ikishindwa kutimiza vigezo hivyo itaweza kufutiwa cheti na hati yake
ya ithibati.
Chuo hicho kilihusishwa na viungo vya binadamu vilivyotupwa
Dar es salaam hivi karibuni baada ya kutumika kwa mafunzo.
Mwisho.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi (26.09.14)
No comments:
Post a Comment