Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC)
Bw. Raymond Mbilinyi (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Bw. Said
Mwambungu muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa baraza la biashara la
mkoa wa Ruvuma katika mkoa huo hivi karibuni. Mkutano huo ulizungumzia namna ya
kuweka mazingira bora ya kufanya biashara ili kuharakisha maendeleo ya
uchumi wa mkoa huo. Katikati ni mtaalamu wa biashara na uwekezaji wa TNBC, Bw.
Willie Magehema.
Na Mwandishi wetu,
Songea
Viongozi mkoa wa
Ruvuma wamehamasishwa kutumia vyema fursa kubwa za uchumi zilizo katika mkoa
huo kubadilisha maisha ya watu wake, kupambana na umaskini pamoja na
kuharakisha maendeleo.
Akiongea wakati wa
mkutano wa baraza la biashara la mkoa huo hivi karibuni, Katibu Mtendaji wa
Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Bw. Raymond Mbilinyi alisema fursa katika
kilimo, madini na utalii katika mkoa huo vitumike kikamilifu.
“Wadau wa sekta ya
umma na binafsi katika mkoa huu wana wajibu wa kushirikiana na kuhakikisha
mazingira ya biashara na uwekezaji yanakuwa mazuri,” alisema.
Alisema kwa sasa
mkoa huo umefunguka na kuunganishwa na mikoa na nchi jirani kutokana na mifumo
mizuri ya barabara zilizojengwa.
“Wana Ruvuma hamna
budi kutumia fursa hii kukuza biashara zenu,” alisema.
Akitoa mfano, Bw.
Mbilinyi alisema kwasasa si tatizo tena kusafiri kwenda na kutoka Ruvuma
kuelekea Mtwara au Mbinga kutokana miundombinu mizuri na kuwa hiyo ni fursa
ambayo inabidi itumike.
Aliwataka
wajumbe wa baraza la biashara la mkoa kufanyia kazi mapendekezo ya mkutano huo
ili yawe na matokeo yanayotarajiwa.
“Mfanyie
kazi vikwazo vilivyoainishwa katika mkutano huu,” alisema.
Katika
mkutano huo, wadau wa sekta binafsi na umma walijadiliana kwa uwazi matatizo
mbalimbali kama kodi, mikopo na mengine ili kuyatafutia ufumbuzi.
“Umuhimu
na upekee wa baraza la mkoa ni kuwa linaunganisha wajumbe wa sekta za umma na
binafsi wanaokaa pamoja na kuamua kuhusu maendeleo…tumieni sana baraza hili,”
alisema.
Kwa
upande wake, mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu alisema ofisi yake
itaendelea kutoa ushirikiano unaotakiwa ili baraza hilo la mkoa lifanye kazi
vizuri na lifanikiwe.
“Tutaendelea
kuhakikisha kuwa tunatoa mchango unaotakiwa ili kufanikisha kupatikana kwa
haraka maendeleo,” alisema.
Alisema ni imani yake kuwa yote yaliyojadiliwa katika mkutano
huo yatapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo
Mamlaka ya Kodi Tanzania (TRA), mkoa; SIDO mkoa, taasisi za fedha, na wadau
kutoka serikalini na sekta ya umma.
Mwisho
No comments:
Post a Comment