Wednesday, September 17, 2014

Kombe la Maghembe lazinduliwa Mwanga

Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro, Profesa Jumanne Maghembe (kulia) akimkabidhi mpira Nahodha wa Timu ya Mwanga FC, Selemani Mwaja muda mfupi kabla ya kuzinduliwa kwa Mashindano ya ligi ya Kombe la Maghembe Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro, Mashindano hayo yanayofanyika katika Uwanja wa Cleopa Msuya kwa mtindo wa ligi inayoshirikisha jumla ya timu 30 kutoka kwenye kata zote za Wilaya ya Mwanga, katika mchezo wa ufunguzi timu ya Mwanga FC ililazwa goli 4 – 1 na Lan’gata FC.

Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro, Profesa Jumanne Maghembe akisalimiana na wachezaji wa timu ya Lan’gata FC muda mfupi kabla ya mechi ya ufunguzi ya mashindano ya Kombe la Maghembe kati ya Lan’gata FC na  Mwanga FC, katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Cleopa Msuya timu ya mwanga FC ilitandikwa goli 4 – 1 na Lan’gata FC.
Na Mwandishi Wetu, Mwanga

Vijana Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kufahamu kuwa michezo ni moja ya njia  kuu inayoweza kuwaunganisha na kuwa kitu kimoja kitakchojenga umoja, mshikamano na amani miongoni mwao.

Akizindua rasmi kombe la Maghembe ( Maghembe Cup),  ambalo limeenda sambamba na uzinduzi wa mfuko wa uwekezaji wa  vijana ( Maghembe Investment Fund) Waziri wa Maji ambae pia ni mbunge wa jimbo la mwanga, Profesa Jumanne Maghembe alisema hiyo ni njia pekee ya kuwakwamua vijana katika makundi yasiyofaa na kujijengea uwezo kiuchumi.

 “Tumeamua kuanzisha mashindano haya kwa lengo maalumu la kuwaunganisha ninyi, si tu katika michezo bali hata katika kujiajiri ninyi wenyewe,” alisema Profesa.

Alisema lengo kubwa la ni kuibua vipaji mbalimbali katika mpira wa miguu, kujenga timu imara katika wilaya hatimae ije kushiriki katika ligi ngazi ya wilaya na hatimae kupata timi bora ya mpira.

“Mkoa wetu kama unavyojua hauna timu katika ngazi ya taifa, huu ni mwanzo wa kujenga vijana, kuwapa ari ya kuona kuwa michezo ni ajira na si kitu cha kupoteza muda,” alisema.

Alisema lengo la pili ni kujenga afya, kujenga mashirikiano, amani miongoni mwao na kuondokana na vishawishi hatarishi katika maisha yao, hii itasaidia kuwafanya wawe na vitu vingi vya kufikiri.

“ Vijana hawa wanahitaji mwongozo katika maisha, na kitu pekee ambacho unaweza ukawaweka vijana pamoja na kuwajengea misingi imara ni kutumia michezo,” aliongeza Profesa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mashindano hayo Idrisa Baja alisema mshindi wa kwanza katika mashindano hayo atajinyakulia shilingi milioni moja pamoja kombe pamoja na piki piki moja, huku mshindi wa pili akiibuka na kitita cha shilingi laki 5 na mipira miwili.

Aidha timu yenye nidhamu itapata shilingi laki 3 na mipira miwili na mchezaji bora wa mashindano atapewa shilingi laki moja.

Mashindano hayo ya kombe la Maghembe, yanayochezwa kwa mtindo wa ligi yanashirikisha jumla ya timy 30 kutoka katika kata zote za wilaya ya mwanga, ambapo fainali zake zitafanyika mwishoni mwa wezi Disemba 2014 katika uwanja wa Cleopa David Msuya.


Mwisho



No comments: