Rais Jakaya Kikwete akiongea na washiriki wa mkutano wa tatu
wa kitaifa wa Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF) hivi karibuni jijini
Dar es Salaam. Waliokaa ni Mwenyekiti wa
Bodi ya ESRF, Bw. Philemon Luhanjo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk.
Hoseana Lunogelo (kulia).
Rais Jakaya Kikwete akiongea na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi
ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF), Bw. Philemon Luhanjo (kulia) na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk. Hoseana Lunogelo (kushoto) wakati wa
mkutano wa tatu wa kitaifa wa Taasisi hiyo hivi karibuni jijini Dar es
Salaam.
Rais Jakaya Kikwete akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF), Dk. Hoseana Lunogelo wakati wa
mkutano wa tatu wa kitaifa wa Taasisi hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Kushoto ni Makamu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Prof. Adolf Mkenda.
Baadhi ya washiriki katika mkutano wa tatu wa kitaifa wa
Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF) uliofanyika hivi karibuni jijini
Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki katika mkutano wa tatu wa kitaifa wa
Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF) uliofanyika hivi karibuni jijini
Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Tanzania inatakiwa kuwekeza zaidi katika watu wake ili kuweza
kufikia maendeleo ya kweli na endelevu.
Imesemekana, kuwekeza katika watu kumethibitisha kuwa moja ya
sababu kubwa ya kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya mataifa mbalimbali
na pia kuwa kati ya mambo muhimu yanayozingatiwa na wawekezaji wanapochagua
maeneo ya kuwekeza.
Hii ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF), Dk. Hoseana Lunogelo alipokuwa akiongea
wakati mkutano wa tatu wa kitaifa wa taasisi hiyo hivi karibuni jijini Dar es
Salaam.
“Kwa kuwekeza katika watu, serikali itahakikisha kuwa
wananchi wanawezeshwa kujiendeshea maisha na kuwa wenye mchango kwa jamii,”
alisema.
Dk. Lunogelo alisema kuwa kuwepo kwa nguvukazi kubwa yenye
ujuzi ni faida kwa wawekezaji wa ndani na nje.
Alisema kuwezeshwa huko kunaletelea ujuzi, maarifa na ufanisi
ambao huimarisha ubora wa nguvukazi.
“Nguvukazi yenye ujuzi ni muhimu sana katika kuhakikisha kuwa
raslimali zinatumika kwa ufanisi, watu wanapata mahitaji yao ya msingi na pia
kukua kwa uchumi,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kwa changamoto za maendeleo
zinazoikabili Tanzania kwa sasa, ni muhimu kuendeleza watu wake ili kuweza
kupambana na changamoto hizo.
Alisema elimu pamoja na afya ya watu kama vitu muhimu
vinavyojenga uwezo na nguvu ya kitaifa kuendeleza uzalishaji na ushindani wa
nchi.
Wakiwasilisha mada kuhusu kuporomoka kwa kiwango cha elimu na
suluhisho lake katika mkutano huo, Prof. Suleman Sumra na Dr. Joviter Katabaro
walisema ni muhimu kwa serikali kufahamu kuwa kuna matatizo na kwamba ni lazima
kuzingatia ubora wa elimu katika mipango na utekelezaji.
“Inawezekana kutoa elimu bora katika shule zetu,” walisema,
na kuongeza kuwa hakuna njia ya mkato isipokuwa kutumia maamuzi yanayotokana na
tathmini na tafiti za kina.
Walisema katika hoja yao kuwa ni muhimu kwa nchi kuzingatia
na kutoa kipaumbele kwa walimu.
“Elimu bora inaweza kupatikana kama tutakuwa na idadi
inayotakiwa ya walimu, waliotayarishwa vyema na wenye motisha,” walisema.
Kongamano hilo lililofunguliwa na Rais Jakaya Kikwete,
lilihudhuriwa na wasomi wa ndani na nje ya Tanzania, maafisa wa serikali, wadau
wa maendeleo, wabunge, mashirika ya kijamii na sekta binafsi.
Tangu kuanzishwa kwake miaka 20 iliyopita, ESRFimekuwa
ikijihusisha na maswala ya sera za kijamii na uchumi pamoja na kutoa ushauri
kwa serikali.
Ikifanya kazi na wadau wengine, taasisi hiyo imeweza
kushiriki katika kutengeneza na kutathmini mipango mbalimbali ya maendeleo hapa
nchini.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya ESRF, Bw. Philemon
Luhanjo alisema taasisi hiyo imefanya kazi kubwa ya kujenga uwezo wa utafiti na
uchambuzi wa sera mbalimbali kwa maendeleo ya nchi.
“Changamoto kubwa tuliyonayo si tu ya maendeleo bali ya
mabadiliko…lazima tuhakikishe kuwa kukua kwa nchi yetu kunaendana na ustawi wa
watu,” alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment