Maofisa kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA), Bw. Geofrey Kobelo na Bi. Loy Mhando wakiongea na mmoja wa
wafanyabiashara mjini Mbeya hivi karibuni. BRELA inaendesha mafunzo kwa
wakazi wa mkoa wa Mbeya kuhusiana na kazi wanazofanya na jinsi wafanyabiashara
wanavyoweza kufaidika na huduma zao.
Msajili Msaidizi wa Makampuni kutoka Wakala wa
Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bi. Rehema Kitambi (aliyesimama)
akiongea na mmoja wa wafanyabiashara mjini Mbeya hivi karibuni. BRELA
inaendesha mafunzo kwa wakazi wa mkoa wa Mbeya kuhusiana na kazi wanazofanya na
jinsi wafanyabiashara wanavyoweza kufaidika na huduma zao.
Na Mwandishi wetu, Mbeya
Wajasiriamali wenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa
mjini Mbeya wametakiwa kuhakikisha viwanda vyao vimesajiliwa na kupata leseni
za uendeshaji, kwani kwa kutofanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.
Rai hiyo ilitolewa mjini humo hivi karibuni na Afisa
Leseni za Viwanda kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw.
Yusuph Nakapala wakati maofisa wa Wakala huo walipowatembelea wajasiriamali katika
maeneo yao ya biashara hivi karibuni mjini Mbeya.
Bw. Nakapala alisema sheria za nchi zinamtaka kila mwenye
kiwanda kupata leseni ya uendeshaji kitu ambacho kitasaidia serikali kupata
taarifa sahihi za viwanda ambazo zitasaidia kupanga mipango na sera za nchi.
Alifafanua pia kuwa faida za kuwa na leseni ni kurasimisha
biashara na kuifanya itambulike zaidi na jamii na taasisi mbalimbali.
“Ukipata leseni ya kiwanda ina maana tayari biashara yako
iko rasmi na inatambulika, na sisi kama serikali tunakutambua kwa biashara
unayoifanya na upo wapi,” alisema.
BRELA
inaendesha mafunzo kwa wakazi wa mkoa wa Mbeya kuhusiana na kazi wanazofanya na
jinsi wafanyabiashara wanavyoweza kufaidika na huduma zao.
Nao baadhi ya wafanyabiashara wenye viwanda vidogo mkoani
humo waliwashukuru maofisa hao kutoka BRELA kwa kuwatembelea na kutoa wito kwa
wajasiriamali wenzao ambao hawajapata leseni kufanya hivyo.
Mmoja wa wajasiriamali hao, Bw. Damas Maghembe alisema
yeye tayari ana leseni ya kiwanda katika biashara ya sabuni anayoifanya na
amepata faida nyingi kutokana na bidhaaa yake kujulikana sehemu kubwa ya mkoa
huo.
“Ukirasimisha biashara yako, unakuwa na mtandao mkubwa na
watu wengine ambao wako mbali…ni rahisi kuendelea,” alisema.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara ambao bado hawajasajili
biashara na viwanda vyao kufanya hivyo kwani kwa kutofanya hivyo kunaikosesha
serikali mapato.
Kwa upande wake, Msajili Msaidizi Mwandamizi wa Makampuni
kutoka BRELA, Bi. Rehema Kitambi alisema waliamua kwenda watembelea
wafanyabiashara katika maeneo yao ya biashara, ili kupeleka elimu ya umuhimu wa
kusajili bidhaa zao kutokana na baadhi yao kukosa muda wa kushiriki semina ya
mafunzo zilizokuwa zikitolewa.
“Wengi wamekuwa wakipiga simu kuwa watakuja kwenye semina
lakini hawafiki, kwa hiyo tukaona ni bora tuwafuate huku huku,” alisema.
Bi. Kitambi aliongeza kuwa mpaka sasa tathmin inaonyesha
kuwa elimu waliyopata
wajasiriamali na wafanyabiashara wa mkoani humo imewasaidia kutokana na
muitikio mkubwa wa wafanyabiashara waliojitokeza kusajili biashara zao.
“Mpaka sasa tumesajili takribani majina ya biashara zaidi
ya 100 kwa wilaya ya Mbeya mjini na Uyole,” alisema. Wilaya nyingine zitakazotembelewa ni pamoja
na Mbalizi na Tunduma..
BRELA
ipo katika mchakato wa kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa kusajili
majina ya biashara popote nchini na nje ya nchi kwa kutumia mtandao.
Mwisho
Mwisho
No comments:
Post a Comment