Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (katikati)
akiwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Bw.
Haji Janabi (kulia) na Mkurugenzi wa Huduma wa kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC), Mama Nakuala Senzia wakati wa warsha ya kujadili matokeo ya utafiti
kuhusu njia za kuongeza uwazi na kukabiliana na rushwa katika mnyororo wa
biashara mipakani mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kulia) akiwa
na mtaalamu mshauri kutoka kampuni ya Gotham International, Bw. John Kyaruzi wakati
wa warsha ya kujadili matokeo ya utafiti kuhusu njia za kuongeza uwazi na
kukabiliana na rushwa katika mnyororo wa biashara mipakani mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Tanzania imeshauriwa kujikita zaidi katika matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuimarisha utendaji wa biashara hasa katika
maeneo ya mipakani.
Imesemekana kuwa pamoja na kuwepo kwa mifumo mingi inayoweza kusaidia
kuongeza uwazi, kupamabana na rushwa na kuleta ufanisi kwenye mnyororo wa
biashara za mipakani, lakini bado mifumo hiyo haitumiki ipasavyo.
Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) imesema wakati sasa umefika kwa
Tanzania kuimarisha matumizi ya mifumo hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye alisema hayo katika
warsha ya kujadili ripoti ya mshauri mwelekezi kuhusu fursa za kuongeza
uwazi na kupambana na rushwa kwenye mnyororo wa biashara za mipakani katika
mwendelezo wa tafiti zilizofanywa na sekta yao ili kuimarisha mazingira ya
biashara hapa nchini.
“Baadhi ya taasisi hapa nchini zina mifumo hii ukiwemo ule wa Tanzania
Customs Integrated System (TANCIS) na ule wa NTBs SMS and Reporting System
lakini hakuna utaratibu unaoiwezesha taasisi zingine kuitumia hasa zile za
maswala ya biashara,” alisema mwishoni mwa wiki.
Alisema mifumo hiyo inawezesha kuweka sheria na taratibu zote za
kibiashara ili watu waione kwa uwazi zaidi na pia husaidia kufanya
mawasiliano yanayolenga kuondoa urasimu na mianya ya rushwa kwa kutoa taarifa
kwa vyombo husika.
Pia utafiti huo umeangalia ni jinsi gani wadau mbalimbali wakiwemo wa
sekta yao wanatumia mifumo hiyo kwa nia ya kuzidi kuweka mazingira bora ya
biashara zikiwemo zile za mipakani.
Akitoa mfano alisema TCCIA imeweza kuweka mfumo wa kutoa taarifa kwa
njia ya SMS popote pale ambapo mtu yupo, hivyo kusaidia kutoa taarifa
mbalimbali zikiwemo za vitendo vya rushwa kwa vyombo kama polisi.
“Matokeo ya tafiti hii yatasaidia kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa
sasa (BRN),” alisema.
Alisema TPSF inapongeza juhudi ya serikali ya kuzidi kuondoa vizuizi
barabarani kwa kiwango kikubwa na kusema kuwa bado kazi kubwa inatakiwa
kufanyika.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Bw.
Haji Janabi, alisema mifumo hiyo ina fursa kubwa katika kuleta mabadiliko
katika utendaji kazi.
“Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika uchumi na utoaji
ajira na jitihada zinazofanyika ni kuhakikisha mifumo hii inafanya kazi kwa
ajili ya kukuza biashara mipakani,” alisema.
Alisema mapendekezo yatakayotolewa kuhusu warsha hiyo yatatumiwa na
serikali hasa wizara hiyo ili kutafuta ufumbuzi katika kuboresha
mazingira ya biashara za mipakani.
Naye mtoa mada katika warsha hiyo, Bw. John Kyaruzi toka Kampuni ya
Gotham International alisema baadhi ya taasisi zina mifumo hiyo lakini hakuna
uratibu wa kuhakikisha inatumiwa na taasisi nyingine.
“Mifumo hii ambayo tayari ipo tukiweza kuwa na uratibu mzuri wa kutumiwa
na taasisi mbalimbali tutapiga hatua kubwa,”alisema.
Alisema TCCIA inatumia mfumo wa NTB SMS and Reporting System na bandari
inatumia mfumo wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) ambayo yote kwa
pamoja ni ya kisasa na ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi.
Naye msimamizi wa utafiti huo, Dkt. Donath Olomi alisema licha ya
baadhi ya tasisi kuwa na mifumo hiyo ambayo ina uwezo mkubwa wa kutumiwa na
taasisi zingine, lakini bado taasisi zingine zinataka kununua mifumo mingine.
“Mifumo hii kuinunua ni gharama sana, mfumo moja unagharimu dola za
Kimarekani milioni 50 sawa na bilioni 70 za kitanzania,”alisema na kuongeza
kuwa hakuna sababu ya taasisi nyingine kununua kwa vile mifumo iliyopo inaweza
kuunganishwa na kutumika kwa shughuli mbalimbali na wengine.
Mwisho
No comments:
Post a Comment