Tuesday, September 9, 2014

Wateja wa Benki ya Afrika Tanzania kufaidika na kampeni

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Wateja wa Benki ya Afrika Tanzania na wale wanaotarajiwa, wanatarajia kufaidika kutokana na kampeni ya benki hiyo ya ‘Weka na Ushinde’ iliyoanza mwezi huu wa Tisa hadi mwezi wa Kumi na Moja mwaka huu.

Akitangaza kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Bw. Solomon Haule alisema wateja wa benki hiyo watajishindia zawadi za papo kwa hapo kama miamvuli, vikombe, fulana na simu za kiganjani aina ya Nokia.

“Wateja watakao fungua akaunti katika benki hii wataingia katika droo la shindano hili na kujipatia zawadi,” alisema, na kuongeza kuwa kwa wale ambao wataweka kiasi cha Tshs milioni 2 na zaidi pia wataingia katika droo hilo na bahati.  

Wakati wa kampeni hiyo, wateja watakaokuwa wanaweka pesa katika akaunti zao watakuwa wamejiweka katika uwezekano wa kupata riba ya hadi asilimia 10 kwa amana za kudumu.

Alisema pamoja na zawadi hizo za papo kwa hapo patakuwa pia na zawadi za kila mwezi zikihusisha vifaa vya kisasa vya mawasiliano vya Tablets, pikipiki, simu za kiganjani aina ya Samsung Smart phones, vocha za mafuta pamoja na vocha za manunuzi.

Mshindi wa mwisho baada ya miezi mitatu ya kampeni anatarajiwa kuibuka na gari aina ya Brevis.

“Kampeni hii inalenga wateja wetu wote na wale wanaotaka kufungua akaunti kwetu,” alisema mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Kampeni hiyo itasimamiwa na bodi inayofuatilia michezo ya kubahatisha Tanzania na itaendeshwa katika matawi yote hapa nchini.

Benki ya Africa Tanzania ilianza huduma zake zaidi ya miaka 30 iliyopita huko Bamako, Mali.

Kwa hapa nchini, benki hii ina zaidi ya miaka saba ikihudumia makampuni makubwa pamoja na kada ya wajasiriamali wadogo na wa kati.

Kwa sasa ina matawi katika mikoa ya Dar es Salaam (yenye matawi kumi), na mengine katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Mtibwa, Mbeya, Tunduma, Mwanza, Kahama na sasa Mtwara.

Mwisho


No comments: