Mtendaji Mkuu wa Wakala wa DART, Bi,
Asteria Mlambo akielezea jambo wakati wa mkutano na wajumbe wa Kamati ya Bunge
ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na maafisa wengine wa
serikali jana jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kushoto ni Manaibu
Waziri, Ofisi ya Waziri mkuu,TAMISEMI, Bw. Aggrey Mwanri na Bw. Kassim Majaliwa
pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Deo Mtasiwa (wa tatu
kushoto). Mkutano huo ulizungumzia maswala mbalimbali ya mradi
unaoendelea wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Hamis Kigwangala
akisisitiza jambo katika mkutano kati ya kamati yake na wakala wa DART
uliozungumzia kuhusu maswala mbalimbali ya mradi unaoendelea wa Mabasi Yaendayo
Haraka (BRT) jana jijini Dar es Salaam. Wengine ni Naibu wake, Bw. John
Lwanji (kulia) na Katibu wa Kamati hiyo, Bw. Yona Kirumbi (kulia).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) imetoa agizo kwa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka
(DART) kuharakisha kufanya makubaliano na Jeshi la Polisi nchini ili kuunda kikosi
maalumu cha ulinzi wa miundombinu ya mradi huo ambayo imekuwa ikihujumiwa na
baadhi ya watu.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Hamis Kigwangala amesema
jijini Dar es Salaam jana kuwa kikosi hicho ni muhimu ili kusaidia kulinda
miundombinu ya mfuno huo wa mabasi ambayo umeghalimu fedha nyingi.
“Tungependa mfumo huu wa mabasi uwe na kikosi maalumu
cha ulinzi ili miundombinu yake isiendelee kuhujumiwa kama ilivyo sasa,”alisema
baada ya kikao kati ya kamati hiyo na uongozi wa wakala wa DART.
Alisema kuwepo kwa kikosi cha ulinzi kutasaidia kwa
kiasi kikubwa kulinda miundombinu hiyo na wale watakaobainika wanahujumu basi
sheria iweze kushika mkondo wake.
Alisema mradi huo umetumia gharama kubwa kuujenga hivyo
ni vyema kila mkazi wa jiji la Dar es Salaam kuchukua jukumu la kuwa mlinzi dhidi
ya wahujumu wa miundombinu hiyo.
Pia alishauri serikali kuzijengea uwezo kampuni za
kizalendo katika sekta ya usafirishaji ili
ziweze kushiriki katika mfumo huo kwa kushirikiana na kampuni za kigeni au
zenyewe.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri mkuu,TAMISEMI, Bw. Aggrey
Mwanri alisema mradi huo kwa sasa unaelekea katika hatua nzuri na wakazi wa Dar
es Salaama watarajie huduma nzuri ya usafiri.