Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wataalamu mbalimbali toka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa
kukutana jijini Dar es Salaam leo katika kongamano la siku mbili
litakalozungumzia kilimo cha mkataba Afrika.
Kongamano hilo limetayarishwa na Chuo Kikuu Mzumbe; Chuo cha
Mipango ya Maendeleo Vijijini cha Dodoma na Idara ya Jiografia na Taasisi ya
Chakula na Uchumi vya Chuo Kikuu cha Copenhagen kupitia mradi unaoangalia fursa
na changamoto za kilimo cha mkataba.
Akitangaza mkutano huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi
wa Mawasiliano, Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Rainfrida Ngatunga alisema mgeni rasmi
anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Chuo hicho na msomi
aliyebobea, Prof. Daniel Mkude.
“Inatarajiwa kuwa kongamano hilo litasaidia katika kujenga
mtandao wa kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusiana na kilimo cha mkataba na
mabadiliko ya maeneo ya vijijini Afrika,” alisema.
Baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na maswala mapya
yanayojitokeza kuhusu kilimo cha mkataba na sera, ufanisi katika uzalishaji,
kilimo cha mkataba, mapato na faida na uzoefu wa kimahtaifa.
Mada zitakazotolewa zitachapishwa katika jarida maalumu la
kimataifa.
Kongamano hilo litamalizika kwa kufanyika kwa mkutano wa majadiliano
ambapo washiriki watapendekeza sera na mambo muhimu yatakayotakiwa
kushughulikiwa na watunga sera.
Kongamano hilo limewezeshwa na msaada wa utafiti kwa Chuo
Kikuu Mzumbe toka serikali ya Denmark kupitia Danish Fellowship Centre.
Mwisho