Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Prof. Adolph Mkenda (kulia) akiwa
pamoja na Naibu
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Fedha na Utawala, Prof. Faustin Kamuzora na
Afisa Mkuu Mtendaji wa Kitengo kinachotoa mafunzo ya menejimenti katika shule
ya biashara ya Chuo Kikuu cha Stellenbosch, Prof. Frik Landman (katikati) mwishoni mwa wiki jijini
Dar es Salaam. Chuo Kikuu Mzumbe
kimefikia makubaliano na Chuo hicho ambapo kozi mbalimbali zitakuwa zinatolewa
katika kampasi ya chuo hicho Dar es Salaam kuanzia mwezi wa Nane mwaka huu.
Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Prof. Adolph Mkenda (kushoto)
akiwa pamoja na Naibu
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Fedha na Utawala, Prof. Faustin Kamuzora mwishoni mwa wiki jijini Dar es
Salaam. Chuo Kikuu Mzumbe kimefikia
makubaliano na Chuo hicho ambapo kozi mbalimbali zitakuwa zinatolewa katika
kampasi ya chuo hicho Dar es Salaam kuanzia mwezi wa Nane mwaka huu. Prof. Mkenda ndie aliyezindua ushirikiano
kati ya vyuo hivyo.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali na sekta binafsi nchini zimesifu ushirikiano mpya wa
kitaaluma uliozinduliwa kati ya vyuo vikuu vya Mzumbe na shule ya biashara ya chuo
kikuu cha Stellenbosch cha Afrika ya Kusini.
Chuo Kikuu Mzumbe kimeingia makubaliano na Chuo hicho kwa nia ya
kutoa mafunzo ya menejimenti kwa maafisa wa serikali na sekta binafsi hapa
nchini na Afrika ya Mashariki kwa ujumla.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa programu hiyo mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba alisema
ushirikiano huo ni hatua nyingine ya maendeleo kwa taifa.
Naibu Waziri huyo aliyewakilishwa na Naibu katibu Mkuu wa Wizara
hiyo, Prof. Adolph Mkenda alisema serikali inakaribisha ushirikiano huo ambao
alisema unaendana na mkakati wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa.
“Watanzania watafaidika na mpango huu ambao masomo yake yatakuwa
yanatayarishwa na wataalamu toka vyuo hivi viwili,” alisema, na kuongeza kuwa
serikali ingependa kuona ushirikiano kama huu zaidi hapa nchini.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni, Dk.
Elisante Gabriel alisema ushirikiano huo umekuja wakati muafaka.
“Nawatakatia mafanikio na ninashauri kampuni hapa nchini kupeleka
maafisa wake kusoma programu hizo zitakazokuwa zinatolewa Mzumbe,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),
Bw. Godfrey Simbeye alikaribisha uhusiano huo na kusema kuwa wadau wa sekta
wanahitaji mafunzo kama hayo.
“Viongozi katika sekta binafsi wanatakiwa kuwa washindani na
program hii inatoa fursa pekee kufanikisha hilo,” alisema.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Kitengo kinachotoa mafunzo hayo katika Chuo
Kikuu cha Stellenbosch, Prof. Frik Landman alisema kama sekta binafsi na
serikali wataona umuhimu, uhusiano huo utakuwa chachu ya maendeleo ya Tanzania.
“Tunafuraha kuwa tunaweza kutoa mchango wetu kupitia njia hii,”
alisema.
Alisema kuwa ni muhimu na kitu cha thamani kwa taasisi katika nchi
zikawa na mameneja wenye ufanisi ili kuweza kuzalisha na kuleta tofauti.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Fedha na
Utawala, Prof. Faustin Kamuzora alisema kuwa uhusiano huo unatokana na mpango
mkakati wa chuo hicho unaolenga kushirikiana na taasisi toka sekta za umma na
binafsi.
Alisema kuwa kuendeleza raslimali watu katika taasisi au kampuni
yoyote ile ni jambo la msingi.
“Hii ni nafasi muhimu kwa taasisi hapa nchini,” alisema.
Kwa mujibu wa mratibu wa mafunzo hayo hapa nchini, Prof. Shiv
Tripathi awamu ya kwanza ya mafunzo hayo itatolewa hapa jijini katika chuo
hicho kuanzia tarehe 28-29 Agosti mwaka huu.
Prof. Tripathi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Kozi fupi na
Ushauri katika chuo hicho alisema mafunzo hayo yatatolewa na msomi maarufu
duniani, Dr. John Westwood aliyekuwa katika shule ya biashara ya Manchester
lakini sasa anaishi Afrika ya Kusini.
Mwisho