Mkurugenzi
wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Mr. Godfrey Simbeye akisisitiza
jambo kwa waandishi wa habari juu ya kuporomoka kwa Tanzania katika viwango vya
dunia kuhusu mazingira ya kufanya biashara. Taasisi hiyo imeitaka Serikali
kuharakisha mchakato wa kuboresha mazingira ya kufanya biashara ilikuvutia
uwekezaji zaidi. Kulia ni Mtaalamu wa Sera wa Taasisi hiyo, Bw. Adam Gahhu.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) imeishauri
serikali kuhakikisha inazidi kuongeza kasi ya kuweka mazingira bora ya ufanyaji
biashara ili kukidhi viwango vya kimataifa na kuvutia uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye
aliwaambia hayo waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa
akizungumzia ripoti ya sasa ya Benki ya Dunia inayoionyesha Tanzania kuporomoka
kwa nafasi 11.
Sasa Tanzania ni ya 145 duniani na ya mwisho katika
ukanda huu wa Afrika ya Mashariki.
“Serikali haina budi kuongeza kasi ya kujenga
mazingira bora ya biashara ili kuvutia uwekezaji,” alisema.
Alisema serikali inawajibu wa kuweka mazingira bora ya
ufanyaji biashara ili nchi isizidi kuporomoka kwenye viashiria vya kimataifa.
Alisema katika kukabili hali hiyo watendaji wa
serikali wanatakiwa kufanya kazi kwa vitendo sababu mazingira bora ya biashara
ndiyo yanavutia uwekezaji na kukuza pato la taifa.
Alisema taasisi yao imeshitushwa na Tanzania
kuporomoka katika uwekeji wa mazingira bora ya biashara na hiyo inaonyesha
watendaji wa Serikali wanashindwa kutimiza wajibu wao.
Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia inaonyesha Tanzania
imeporomoka kutoka nafasi ya 134 mwaka 2013 hadi nafasi ya 145 kati ya nchi 185
katika kuweka mazingira bora ya biashara ili kuvutia uwekezaji.
Alisema ripoti hiyo inayotolewa kila mwaka na benki
hiyo inaonyesha kuwa Tanzania inazidi kushuka kwa miaka mitatu mfululizo.
“Ripoti hii imeishitua taasisi yetu na imetusikitisha
sana kwa sababu badala ya kupanda tunashuka...na safari hii tumeshuka kwa
nafasi 11 hali ambayo si nzuri kwa uchumi wa nchi,” alisema.
Benki hiyo inapima hali ya nchi ya ufanyaji biashara
kwa kuangalia viashiria vilivyowekwa kimataifa vikiwemo utoaji wa vibali vya
ujenzi.
Viashiria vingine ni pamoja na upatakanaji wa umeme,
kuandikisha rasilimali, upatikanaji mikopo, ulindaji wawekezaji, mifumo ya
ulipaji kodi, namna ya kufanya biashara za mipakani, kuingia mikataba, kufungua
na kufunga biashara na kuajiri wafanyakazi.
Ripoti inaonyesha viashiria hivyo havija weza
kutekelezwa kwa kasi inayotakiwa na serikali ili kuhakikisha Tanzania inapanda
kutoka pale ilipo.
Pia ripoti hiyo inaonyesha nchi nane bora Kusini mwa
Jangwa Sahara zinazofanya vizuri ni pamoja na Mauritius ya 20, Rwanda ya 32,
Afrika Kusini ya 41, Botswana ya 56, Ghana ya 67, Zambia ya 83, Morocco ya 87
na Namibia ya 98.
Alisistiza kuwa katika mpango wa kufikia uchumi wa
kati mwaka 2025, ni vyema jambo hili likawa katika vipaumbele vya serikali ili
kuzidi kuvutia biashara na uwekazaji.
Alisema Rais Jakaya Kikwete mwaka 2009 aliagiza kazi
ifanyike na vikosi kazi viliundwa ili kufikia vigezo hivyo, lakini kasi
haijawa kubwa kutokana na wahusika waliopewa dhamana hiyo kutotimiza vyema
wajibu wao.
Pia alisema vikosi kazi vilivyoundwa katika
kuhakikisha jambo hilo linatekelezwa vinakabiliwa na changamoto ya
kutokutana maranyingi, kutoweka vipaumbele na ufinyu wa bajeti.
Kwa Upande wake Mchambuzi wa Sera wa taasisi hiyo, Bw.
Adam Gahhu alisema taasisi yao inahitaji kuona serikali inaongeza utendaji na
uwajibikaji ili Tanzania iweze kujiondoa katika nafasi hiyo mbaya.
Alisema kupitia “Matokeo Makubwa Sasa” ni vema
serikali ikatumia kutumia fursa hiyo kuweka mazingira bora ya bishara ili
kusaidia kuvutia uwekezaji kwa uchumi wa nchi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment