Thursday, November 28, 2013

RUBADA yawataka maafisa ugani kuwa wabunifu

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja akizungumza na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Morogoro wakati wa semina ya mafunzo kuhusiana na mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa na Kilimo Kwanza hivi karibuni Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw. Said Amanzi (katikati) akizungumza na watendaji wa ngazi mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro wakati wa semina juu ya mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa na Kilimo Kwanza hivi karibuni Morogoro. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji  (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja, na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Bi. Kibena Kingu.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) imewataka maafisa ugani katika halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini, kuwa wabunifu katika utendaji wao wa kazi ili waweze kuongeza thamani ya mazao, pamoja na kutoa elimu stahiki kwa wananchi wanaowatumikia.

Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA, Bw. Aloyce Masanja alitoa ushauri huo katika halmashauri ya  Wilaya ya Morogoro Mkoani humo wakati wa semina elekezi kwa watendaji wa halmashauri hiyo juu ya mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa ( BRN) hivi karibuni.

“Ni vyema maafisa ugani wakaelewa kuwa wao ndio viongozi katika suala la kutoa maelekezo kwa wananchi wao,” alisema.

Alisema maafisa ugani waliopo ni wachache kulinganisha na mahitaji yaliyopo katika vijiji, hivyo kazi kubwa iliyopo ni kujaribu kuwapa elimu ili waendane na mfumo uliopo na mahitaji ya wakati.

“Tumekuwa na wagani wachache katika vijiji, japo wanafanya kazi lakini wamekuwa sio mfano bora kwa wale wanaowatumikia, kutokana na wao wenyewe kutojishughulisha na kilimo na ndio maana hata wananchi wamekuwa na hamasa ndogo juu ya suala la kilimo,”alisema Masanja.

Aliongeza kuwa utamkuta afisa ugani hana hata shamba au mfugo japo mmoja tu jambo linalosababisha wao wenyewe kutokuwa na mwamko katika sekta ya kilimo na mifugo katika vijiji wanavyofanyia kazi.

Akizungumzia suala la upungufu wa maghala ya chakula katika wilaya ya Morogoro vijijini, Bw. Masanja alisema tatizo hilo linatokana na kuwepo na maghala ya zamani na ambayo hayana viwango vya kuweza kuhifadhi chakula.

“Katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa tunataka kila kijiji kiwe na kilimo cha umwagiliaji na patajengwa ghala la kisasa kwa ajili ya kuhifadhia chakula,” alisema.

Alisisitiza kuwa kwa sasa kuna upotevu mkubwa sana wa chakula hasa mpunga na mahindi kutokana na kutohifadhiwa katika maeneo maalumu, hivyo kusababisha njaa zisizokuwa za lazima katika maeneo kadhaa ya wilaya hiyo.

“Watu hawana ufahamu wa uhifadhi, chakula kimekuwa kikiwekwa chini…ni muhimu swala hili lirekebishwe,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.

Akizungumzia swala la usindikaji katika wilaya hiyo, alisema watu wamekuwa wakiuza mazao kiholela bila kuyafanyia usindikaji, jambo ambalo limekuwa likiwasababishia kukosa soko la kueleweka na hivyo kukosa kipato cha kujikimu.

“Chakula kingi kinauzwa kama kilivyo, badala ya kuuza mchele tunauza mpunga, na badala ya kuuza unga tunauza mahindi, hili ni tatizo kubwa kwa wakulima,” alisema.

Aliwataka watendaji kuwaunganisha wananchi wao katika vikundi na kuunda umoja wao, ili wawe na mashine za kukobolea jambo litakalokuza soko la mazao yao na kuongeza thamani.

Kwa upnde wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bw. Saidi Amanzi, alisema serikali ina nia nzuri ya kuwakomboa wananchi wake kiuchumi, hivyo ni vema wakaunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali yao.

“Sisi upande wa serikali tunajitahidi kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala la kilimo chenye tija na kitakachomkomboa mwananchi,” alisema Amanzi.

Aliongeza kuwa Wilaya ya Morogoro hasa maeneo ya vijijini wamehamasika kwa kiasi kikubwa na mipango mbalimbali ya serikali ya kukuza kilimo katika maeneo hayo.

Mwisho 


No comments: